
Adeladius Makwega-MBAGALA
KIZINGA
Mwanakwetu alikuwa na binamu yake mpendwa aliyefahamika kama Alphonsina ambaye anazaliwa na shangazi yake mkubwa. Alphonsina alikuwa akisoma Shule ya Msingi Miburani iliyopo Temeke Dar es Salaam. Mara nyingi Mwanakwetu alikuwa akienda kumsalimia binamu yake huyo ambaye sasa ni marehemu. Safari za kutoka Mbagala kwenda Temeke zilisaidia Mwanakwetu kufahamu mengi juu ya Wilaya ya Temeke na hata siasa za Tanzania, maana Temeke hadi kesho ni wilaya yenye masikini wengi.Mambo aliyofahamu Mwanakwetu hapo Temeke ni mengi kwanza ni uwepo wa kibanda kimoja cha biashara ambacho kilikuwa kinauza kanda za Kaseti za dini ya Kikristo ambapo nyimbo kadhaa ya Wakristo hasa Waprotestanti zilikuwa zikuuzwa na kuchezwa siku nzima.
Mojawapo wa wauzaji na wamiliki wa kibanda hicho alikuwa ni huyu Baba Askofu Zakaria Kakobe, kwa hakika nyimbo hizo za dini nyingi zilikuwa hazichezi Redio Tanzania Dar es Salaam lakini mitaani zilikuwa zinachezwa sana ikiwamo nyimbo za Wanamuabudu Nani? Na Malebo za Mchungaji Faustine Munishi. Jambo la kustajabishi nyimbo hizo za dini ya Kikristo karibu zote ziliweza kuchezwa na KBC-Taifa ya Kenya katika vipindi vya dini na hata katika makala kadhaa za Shirika hilo la Utangazaji la Kenya.
Kwa hiyo Mwanakwetu mara nyingi alfajiri alikuwa akifungua KBC Taifa kwa kuwa alivutiwa na nyimbo hizo za Kikristo maana kununua kaseti hakuwa na pesa hiyo na hata redio kaseti ya kuzichezea hakuwa nayo. Kwa hakika nyimbo hizo ambazo nyingi zlirekodiwa Kenya mathalani Wanamuabudu nani? zilikuwa zikirusha madongo kwa Kanisa Katoliki, Mwanakwetu kama Mkatoliki pale kwenye ukakasi kibindamu alikuwa akivumilia tu huku akivutiwa na vipande ambavyo havikuwa na ukakasi kwa imani yake. Msomaji wangu hapo Temeke jirani na Shule ya Msingi Miburani kulikuwa na Kibanda cha wachoraji maarufu sana waliofahamika kama Black Wizard ambao walikuwa wakichora michoro mbalimbali katika sehemu za biashara mabango, nyumba, magari na vifaa vingine hawa jamaa walikuwa maarufu sana.
Katika banda hilo la Black Wizard lilikuwa linamilikiwa na Wandengereko wa Kilimahewa Mkuranga Pwani ambapo walikuwa wakifanya kazi kidugu na kirafiki na mmojawapo wa wachoraji wa Black Wizard alifahamika kama Nasser Swalehe, huyu ndugu alikuwa akifahamiana kwa karibu na binamu wa Mwanakwetu aitwaye Alphonsina na hata Mwanakwetu alipokuwa akienda kumsalimia dada yake Shuleni ya Msingi Miburani jamaa huyu alikuwa akimuhoji dada wa Mwanakwetu juu ya ugeni huo, Alphonsina alimtambulisha Mwanakwetu wa Nasser hivyo hilo likajenga ujirani na jambo hilo likafanya Mwanakwetu kila alipoenda Shule ya Msingi Miburani mara zote alikwenda kumgoja binamu yake huyu katika Kibanda cha Black Wizard .Maswali ya Nasser kwa Alphonsina binamu wa Mwanakwetu yalimkera mno Mwanakwetu.
“Wandengereko siyo watu wa vitendo, ni watu maneno mengi vitendo hakuna, unauliza maswali juu ya binamu wa Mwanakwetu wakati posa haujatoa na tukikwambia tukubatize hautaki, sasa usiulize maswali na usiwapende dada wa Mwanakwetu.”
Hapo Mwanakwetu akafahamiana kwa karibu na Nasser kwa kuwa Mwanakwetu alimpa sindano za moto waziwazi huyu ndugu na kuwa salama, Nasser alijenga urafiki na Mwanakwetu na hilo likajenga urafiki hata na mdogo wake aliyefahamika kama Hamidu.
Miaka inasonga baadaye hawa jamaa wa Black Wizard wakawa na tenda ya kufanya promesheni ya bizaa mikoani hivyo shughuli za uchoraji zilizowapatia pesa kidogo zikawekwa kiporo lakini Nasser kutokana na kumpenda sana binamu wa Mwanakwetu akakataa kwenda mikoani Nasser na Hamidu wakaamua kufungua ofisi yao Mtoni Relini kando ya Msikiti wa Maboksi na huku Black Wizard ikibaki na vijana wadogo wasio na ujuzi mkubwa wa kuchora.
SELEIMAN HEGGA
Baadaye Alphonsina dada wa Mwanakwetu aliyekuwa nakaa na Baba yake Mzazi Temeke Kotta akafariki dunia kwa shida ya uzazi wakati wa kujifungua kama nilivyoeleza hapo juu naye Mwanakwetu muda huo anamaliza kidato cha sita mwaka 1998, wakati wa kungoja matokeo ya kidato cha sita Mwanakwetu akawa anashinda Mtoni Relini Kando ya Msikiti wa Maboksi kulikuwa na biashara za binti Makwega, Mtoni Relini karibu na Tawi la CCM Mtoni Sokoni ambapo mara zote tangu saa tatu asubuhi hadi usiku wazee wa CCM hucheza Bao.Hapo hapo Mwanakwetu akakutana na Nasser hapo keshaoa wamama wawili na sasa alikuwa ni Imamu wa Msikiti wa Maboksi kwenye safu ya uongozi ana cheo.
Mwanakwetu akamwambia Nasser,
“Umesubiri binamu yangu afe ndiyo uoe Waisilamu wenzako.”
Nasser mtu muungwana akawa anasikitika tu akisema Makwega ile ni kazi Mungu.Hapa Mwanakwetu akakutana na Nasser Swalehe na Hamidu Swalehe ndugu katika ofisi yao ya uchoraji isiyo na jina , ofisi kuukuu, ofisi ,chafu maana hawakuwa na mtaji mkubwa.
Kumbuka Mwanakwetu anafahamiana na Nasser na Hamidu kupitia binamu yake Alphonsina tangu miaka ya 1980 mwishoni pale Temeke Miburani katika ile kampuni ya uchoraji ya Black Wizard, baadaye Alphonsina alifariki kwa uzazi na kuzikwa, sasa Mwanakwetu yu Mtoni Relini hapo hawa jamaa wakawa kama ndugu zake huku wakimtania Mwanakwetu kwa mambo manne; kwanza ule ushemeji na binamu yake aliyefariki dunia Alphonsina, pili utani wa Aya za Biblia za Paulo Mtume kumbuka kipindi hicho ndipo mihadhara ya dini ya ushindani mkubwa baina ya Ukristo na Uisilamu ilikuwa inafanyika na aya anayoikumbuka Mwanakwetu ni ile Wagalatia 3,1-14
“Enyi Wagalatia, msio na akili ni nani aliyewaloga,ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu amesulubiwa? Nataka kujifunz neno hili moja kwenum Je mlimpokea roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! m mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho mnataka kukamilisha katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.Basi, yeye awapaye roho na kufanya miujiza kati yenu, je afanya hayo matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?...”
Jambo la tatu ambalo nalo lilijenga mahusiano haya zaidi ni utani kuwa Nyangu Omella, na Aloyius Romanus Mnyeke na Mwanakwetu ni walaji wazuri wa Mkuu wa Meza Nyama ya Nguruwe na jambo la nne sote tulikuwa wana CCM wa Tawi la CCM Mtoni Sokoni.
Msomaji wangu haya maisha yaliendelea vizuri na mwaka 1999 Jimbo la Temeke kulifanyika uchaguzi wa mbunge baada ya Augustine Mrema kupigwa mizengwe na yeye kuhama NCCR na kwenda TLP., jimbo likawa wazi uchaguzi ukatangazwa, kampeni zikaanza kwa hiyo Mwanakwetu , Nasser na Hamidu waliweza kuifuatilia mikutano mingi ya uchaguzi huo wakiongozwa na Katibu wa CCM wa tawi hilo dada mmoja mrefu mnene mweusi jina lake limesahaulika.
Hapo sasa asubuhi kila mmoja anatekeleza majukumu yake na jioni kwenye mikutano ya kampeni, katika uchaguzi huo yupo mgombea mmoja hakuwa anafahamika na Mwanakwetu kwa karibumaana wagombea wote vyama vikubwa Mwanakwetu alikuwa anawafahamu kwa karibu na jambo hilo likasababisha Mwanakwetu ashiriki katika mojawapo ya mkutano wa kampeni. Wagombea wa ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi huu ninaowakumbuka walikuwa wafuatao; John Makombe KIbasoo (CCM) akitokea kata ya Kurasini awali kama diwani, Abbasi Mtemvu –TLP, Richard Hiza Tambwe (CUF) na Seleiman Hegga (NCCR-Mageuzi) ambapo hiki chama ndicho kilikuwa chenye jimbo hilo kabla ya Mrema kuukacha ubunge.
Ninachokumbuka huyu diwani wa Kurasini John Makombe Kibaso niliwahi kumtania nenda kagombee kwenu Musoma akawa anacheka akisema yeye Kurasini ni kwao kaja akiwa mdogo. Wagombea hao wanne kutoka vyama maarufu Seleiman Hegga peke yake nilikuwa sijawahi kumuona kwa karibu japokuwa nilikuwa namsikia redioni pale RTD na baadaye BBC.
Mwanakwetu alihudhuria mkutano wa NCCR uliofanyika Shule ya Msingi Mtoni Mama Mere jirani na darasa linaloonekana la kwanza kama unakwenda Mbagala, huku siku hii Mwanakwetu aliambata na Nasser na Hamidu wale ndugu zake.
Marehemu Suleiman Hegga ambaye alizungumiza ya juu kifo cha Sokoine yeye akiwa RTD kama Mkuu wa Vipindi na changamto za RTD baada ya msiba huo ikiwamo Kipindi cha Mikingamo hadi kikapoteza muelekeo. Kwa wasomaji wenye umri mdogoo kipindi cha Mikingama kilikuwa kinawafichua wale wanao hujumu uchumi na kilimuongezea nguvu kubwa marehemu Edward Moringe Sokoine.
“Nawaambieni Edward Sokoine Alifariki na kuzikwa na Kipindi chake cha Mikingamo.”
Seleiman Hegga alizungumzia hili ;
“CCM ni mtoto wa ASP(MAPINDUZI) na TANU(MAZUNGUMZO) kwa hiyo CCM wanaweza kutumia mazungumzo kufanikisha jambo loloye kwa 50 asilimia na wanaweza kuligeuza jambo kwa 50 asilimia , kwa CCM siyo 100 mazungumzo lakini vyama vilivyoanza mwaka 1992 ni mazungumzo 100 asilimia lazima Tanzania waelewe uhitaji wa chama kipya kutawala hili taifa. Kwa hiyo nafasi ya chama kipya kuiongoza Tanzania ni muhimu. Mkutano wangu mpo watu wachache njoni msitukilize hapo mpo watu wachache sana timieni hii fursa vizuri.”
Msomaji wangu hapo Mwanakwetu katoka kuhitimu HKL kwa huku akinoti maelezo ya Mzee Hegga mkutanoni.Katika mkutano huo Mwanakwetu alimuuliza maswali kadhaa ndugu Seleiman Hegga ambayo maswali hayo ameshawahi kuyasimulia katika simulizi kadhaa za huko nyuma.
Mkutano huu ulikuwa na watu wachache mno wasiozidi 20 ambapo hapo hapo kulikuwa ana viongozi wa NCCR Mageuzi na wasikilizaji akiwamo Mwanakwetu, Seleiman Hegga alikuwa na gari yake ndogo ya rangi Silva ikiwa imebandikwa karatasi zake za kuomba kura.Mkutano huo wa kampeni ulipokwisha tukarudi nyumbani.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika urafiki wa Nasser , Hamidu na Mwanakwetu ni wa miaka mingi uliojengwa na mahusiano ya binamu yake Alphonsina na ukajenga udugu huo huku wakitaniana mambo mengi hadi ya dini bila ya kugombana huo ndiyo Utanzania kw ahiyo tusikubali mjinga yoyote atugombanishe na hata haya mambo ya watu wasiojulikani huu sio Utanzania, anayetaka kuyaendeleza mabo ya watu wasiojulikane atengeneze taifa lake
Je wewe msomaji wangu urafiki wako na mnaolewana nao umejengwa na nini?
Kwa hakika jibu utakuwa nalo.
Shabaha ya pili ya makala
haya, Seleiman Hegga alizungumzia juu ya CCM kuwa zao la ASP na TANU, CCM sasa
inawajibu kwa kujitahidi mno kushugulikia
masuala ya Watanzania masikini kufa na kupona ili kulinda uwepo wao kisiasa,
mema yanapaswa kuendelezwa mabaya yawekwe kando.Usipokuwepo umakini dhana ya Seleiman Hegga itakuwa sahihi.
Shabaha ya tatu ya makala haya, kulingana na maelezo ya marehemu Seleiman Hegga katika mkutano ule pale Mtoni Mama Mere, kifo cha marehemu Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo alizikwa na falsafa yake ya mapambano na wahujumu uchumi.
“Kipindi cha Mikingamo kilisuasua sana na baadaye kufilia mbali na sie kwenda Ughaibuni.”
Kwa haya maelezo ya mtangazaji
Seleiman Hegga yeye mwenyewe hakulidhishwa kabisa na mazishi ya falsafa ya
Edward Moringe.Sokoine m Sokoine kazikwa mwili falsafa yake lazima viongozi wetu waindeleze kwa namna wanavyoishi katika maisha yao iwe ofisni na majumbani mwao kila siku inayokwenda kwa Mungu wanapoliongoza hili taifa maana falsafa haizikwi.
Mwanakwetu anaamini jukumu
la Tanzania ya sasa siyo kukaa na kuandika vitabu vya Edward Moringe tu kuvizindua
na kuviweka maktaba bali wajibu wa kila viongozi wakuu wa Tanzania kuishi
maisha ya falsafa za Edward Moringe Sokoine ili wananchi wa Tanzania waige.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
Viongozi Waishi Falsafa ya Edward Moringe.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment