Adeladius Makwega-MBAGALA
Msomaji wangu huu ni wasaa mwingine wa kukualika tena katika makala ya katuni ambayo ni mjumuiko wa katuni nne zilitoteuliwa na mtayarishaji wetu na kuingizwa katika kapu la makala haya siku ya leo.
Kuyaanza makala haya Mwanakwetu ameikamata katuni inayoonesha mandhari mbili; mojawapo ni wakati mgao wa umeme umeishika hatamu KUU na chini yake wakati mgao wa umeme umeshika hatamu NDOGO.”
Msomaji wangu hizo ni habari za hatamu mbili. maana bado umeme unakatikakatika. Katika mchoro wa hatamu kuu kunaonekana ndoo kadhaa za maji zimepangwa kando ya foleni na mbele kuna bomba ambalo halitoi maji na kando kuna jamaa kalala kapewa jina mamlaka, kibosile huyu akisema hakuna maji kwa sababu ya mgao wa u meme na kwa chini kuna mchoro unaonesha hatamu ndogo, hii ni mandhari kama hiyo hiyo ya awali na wao wahusika wa maji wana Lori lao lasambaza maji, jamaa wahusika na maji wanasema kuna shida ya loo presha .
Kwa hakika waziri anayeshugulikia Maji wa Tanzania ni rafiki na ndugu wa Mwanakwetu ndugu Jumaa Aweso- wewe mtu mwema, wewe ni mtu mwaminifu na wewe ni mpenda maendeleo na natambua unaipenda kazi yako ya uwaziri na nchi yetu, shida mheshimiwa ni kupata maji kikubwa kwako wahimize waliochini watumize majukumu yao, hasa hizi mamlaka za maji tupate maji, mathalani Mheshimiwa Jumaa Aweso mimi nipo hapa Malya mkoani Mwanza nilishahau kuyaona maji ya Bomba, mwendo ni maji ya Bwawani na viluiui tu na ukiuliza juu ya hilo stori nyingi sana. Mita zimefanya hivi na vile. Mh Aweso na wizara yako yote, kwa hili Mwanakwetu ninawaambia tu Wabilahi Tawfiki .
Katuni hii ya UKAME wa maji safi na salama inaufungua mlango wa kuikamata katuni ya pili inaoonesha mrembo mmoja aliyechora vizuri mithili ya Faraja Kotta mshindo wa Taji ya Miss Tanzania mwaka 2004, ambaye n mrembo kweli kweli lakini urembo wa Faraja Kotta msomaji wangu haujaufikia hata robo ya urembo wa mama yake mzazi Mwalimu Margereth Kotta ambaye aliwahi kumsomesha Mwanakwetu pale Tambaza sekondari. Mwalimu mwingine mrembo pale Tambaza alikuwa Mwalimu Mdemu, ndiyo kusema msomaji wangu Faraja Kotta kadokoa sehemu ndogo sana ya urembo wa mama yake mzazi ambapo mashahidi wa hili ni wanafunzi waliopata bahati ya kusomeshwa na Mwalimu Margereth Kotta pale Tambaza enzi hizo . Hizo ni habari ya Madaam Kotta na pale Tambaza- sasa turudi katika makala ya katuni, huyu mrembo kapewa jina uchaguzi Serikali za Mitaa, mkono wa shoto anapotazama mrembo huyu CCM wanamuhonga zawadi na mkono kuume CHADEMA pia nao wanamuhusudu mrembo huyu na kazawadi kando, sasa mrembo huyu sijui atapokea zawadi ya nani? Je CCM au CHADEMA ? Kwa hakika Mwanakwetu hana jibu, kikubwa kwa wapiga kura kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 na kwa siku hii Mwanakwetu atapiga kura Kituo chake cha Kizinga Mbagala .
Msomaji wangu,
“Watu walikuwa wanatuonea gere kusomeshwa na Mwalimu Margereth Kotta, maisha haya ! Siku zinasonga.”
Katuni hii ya mrembo wetu iliyomkumbusha Mwanakwetu mwalimu wake Madamee Kotta inanipa nafasi ya kuikamata Katuni ya tatu inayoonesha mwanahabari akikata mbuga akiwa na kamera tele , noti buki , peni na vifaa vya kazi kedekede na vingine vimemdondoka, huku akipiga hatua na kuruka vihunzi kadhaa kama vile Uhuru wa Kujieleza –Katuni hii imemkumbusha Mwanakwetu mjadala wa wanahabari katika kundi moja uliofanyika Oktoba 1, 2024 wakisema,
“Jamani uhuru wa kujieleza haupo, wapo wanaonakili maoni yetu na kuyapeleka kunakohusika haraka.”
wakiwataja wanahabari waliowahi kupata changamoto mathaani Erick Kandera. Kikubwa Mwanakwetu anaomba wenye mamlaka watoe nafasi ya vyombo vya kufanya kazi kwa uhuru ili wananchi watoe maoni yao na jamii ipate kile kinachostahili kutoka katika vyombo vya habari vya Tanzania.
Katuni hii ya Mwanahabari na vifaa vyake akipiga hatua katika vikwazo tele inatoa nafasi ya kuikamata katuni ya nne inayomuonesha mama mmoja aliyevaa hijabu maridadi ya rangi ya njano na sare za CCM, mama huyu anasema-Jamani jibuni hoja msiogope wakisema nimeua-Jibuni nimeua UPINZANI sijawahi ua hata SISIMIZI.
Mwanakwetu anatumia katuni hii kukumbusha mambo kadhaa ambapo CCM imeyaahidi katika uchaguzi mkuu wa 202O ndani ya ilani yake hasa sura ile ya tano juu ya Ulinzi na Usalama na Sura ya Sita juu ya Utawala Bora, jambo hilo limesisitizwa sana na kwa kina kwa hiyo viongozi katika Serikali wanaotokea CCM katika nafasi za dola wanawajibu wa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha sura hizo mbili za ilani zifanyiwa kazi kikamilifu bila kumuona aibu mtu au idara yoyote maana hicho ni kiapo cha CCM kwa mpiga kura. Mwanakwetu anakumbusha kurasa wa awali wa ilani ya CCM ya 2020-2025 kuna maneno haya,
“CCM inatambua kuwa Serikali inazoziongoza zina jukumu la kuhakikisha walio wanyonge wanapata fursa na kipao mbele cha kustawi katika maisha yao.”
Hapa Mwanakwetu anasema utekaji, udhalilisha na mauwaji hayaleti ustawi wowote kwa jamii yetu.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka tu - Faraja Kotta na Robo ya Urembo wa Mama Yake
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail. com
0717649257
Post a Comment