
Adeadius Makwega-MWANADILATU-PWANI
Tangu mapema ya mwaka 2024 Mwanakwetu amepokea simu kadhaa kutoka kwa ndugu zake wa Pwani, Dodoma na Dar es Salaam akikumbushwa kutembelea maeneo hayo maana mwaka huo kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, viongozi hao wa vijiji na mitaa wanachaguliwa upya.
Mwanzoni jambo hilo halikuwa na maana kwake lakini ilipofika Septemba akakata shauri na safari hizo huko Dodoma, Dar es Salaam na Pwani mikoa iliyopo Tanzania, taifa lililopo Afrika ya Mashariki.
Awali huko Pwani eneo la Mwanadilatu anapoishi
ndugu Iddi Ramadhani Rangweni alimwambia Mwanakwetu maneno haya;
“Kaka ninakuheshimu sana, huku sasa ardhi ni mali, ukichelewa utakuta shamba lako lote limekatwa viwanja, huku kiwanja kimoja hadi milioni kumi, sasa siyo ile ya Mwana-dila-tuu miaka ya Mwalimu Francis Makwega na Mwalimu John Kiondo! Njoo kaka, nakuheshimu sana na ndiyo maana nasisitiza hilo.”
Mwanakwetu akatoka Mwanza hadi Mwanaladilatu na mapema sana ya siku hiyo na alipofika huko akakutana na Mzee Iddi Rangweni alafu akaongea na nduguye Kitindi Rangweni ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM wa Kata huko Mwanadilatu wilaya Mkuranga mkoani Pwani. Hapo hapo habari za siasa za Mkuranga ziliulizwa jamaa wakasema aaah hawajamuona mtu mwingine wao wanamuunga mkono Abdalah Ulega. Hapa Mwanakwetu akasema kumbe nyota ya Ulega inang’aa.
Baada ya mazungumzo hayo Mwanakwetu na Iddi Rangweni kigulu na njia hadi Kitongoji cha Nasako ambapo Mwanakwetu ana ardhi yake, walipofika hapo alibaini kuwa eneo lake kama nusu ekali lilimemegwa na ndugu mmoja kutoka mkoa wa Mara aitway e Rosana Marwa na jamaa huyu alikwenda mbali na hapo akamzika mdogo wake. Marwa nayeye alipofika hapo huku akitoa maneno makali, Iddi Rangweni akasema.
“Makwega jirani yako ndiyo huyu leo hii tulimalize suala na mipaka yetu maana wote watatu tupo .”
Huyu Marwa sehemu ya ardhi yake inapakana na Mwanakwetu pia inapakana na watoto wa marehemu Ramadhani Rangweni ambaye alifariki mwaka 1985 ambaye ni baba wa Rangweni Iddi na Rangweni Kitindi na ukoo huo ndiyo uliyoiuzia familia ya akina Makwega.
Baadaye alifika mwenyekiti wa Kitogoji wakaliweka sawa, lakini kumbuka Mkurya keshazika nduguye hamuwezi kuifukua maiti iliyolala kaburini, ayefariki hana kosa na hata aliyemchukua hana kosa, jambo hilo likaisha vizuri na maiti haikufukuliwa.
“Makwega si umeona tunavyopata lawama? Mimi nimezaliwa hapa mwaka 1970 na mwaka 1972 mzee wangu Ramadhani Rangweni akanipa mti wa muembe niupande ule paleee, kando ya makaburi yetu. Haki ya Mungu ningekuwa mimi sipo hapa, hii ardhi ungeshadhulumiwa mchana kweupe, siku nyingi, mimi sitaki kufa na dhambi hiyo? Lakini sasa jamani jua hili kali twendeni tukapumzike kando ya makaburi katika ule muembe wangu niliyopanda, baadaye tuanze kurudi Mlamleni.”
Kwa bahati nzuri tulipofika hapo tukapumzika, tukiwa watu wanne jamaa mmoja Mpogolo, Mwanakwetu, Iddi Rangweni na mtoto kama wa miaka kati 7-9 nadhani ni mtoto wa mwisho wa Iddi Rangweni.
Hapo Mwanakwetu akaoneshwa ule muembe wa mwaka 1972, muembe huu ninaufahamu miaka mingi maana watu wakichoma moto huwa unaungua lakini baadaye unachipua, tukiwa hapa simulizi zinaendelea,
“Kuna taperi mmoja siku moja nipo nipo bustanini kwenye bwawa lako, naona kundi la watu, wakafika hadi makaburini wakinamama wakiwa wengi , hayo sasa majira ya saa nne ya asubuhi, nikatulia kimya nione kinachoendelea, wamevaa kaniki na vilemba, jamaa akawa anachota maji katika bwawa lako anawaongesha na nguo zao mmoja baada ya mwingine kundi lote, siku hii nilikuwa nimefunga Ramadhani, wakamaliza na baadaye kuondoka na kundi lile. Jioni nikamfuata nyumbani kwake yule mganga nikamwambia akome kufanya upuuzi wake katika makaburi ya familia yetu na kama nitamuona tena nitamshikisha adabu.Yule mjinga sana, natambua anaweza kuwa bado anakuja hapa kwa siri.”
Kumbuka tupo tumepumzika makaburini, jua kali mno baada ya kutatulia mgogoro wetu, huyu kijana mdogo anaogopa hizo simulizi anatetemeka.
Hapo hapo Idd Rangweni akaamka, kumbuka baada ya kupumzika kwa muda huku akaanza kuondoa majani katika makaburi, akaanza la baba yake yaani Ramadhani Rangweni aliyefariki 1985 ambalo ni kaburi kongwe huku akawa anaondoa majani makavu na mabichi kwa mikono akafika katikati ya kaburi akasema,
“Si unaona hawa jamaa walivyo washenzi katikati ya kaburi la baba yangu wamekiweka chungu? Akakifunua na ndani yake kikuwa kimefunikwa kidaka”
Kwa wale wasomaji wangu ambao siyo wazaliwa wa Pwani ya Tanzania, naomba nieleze juu ya neno KIDAKA
“Kabla ya Nazi kuwa nazi kwanza inatoka kwenye Kitale, Kidaka alafu Dafu ndiyo Nazi alafu Mbata. Makabila ya Pwani ya Tanzania wanakitumia Kidaka kikidondoka mnazini huwa kama chaki na kuandikia, misemo, methali , ujumbe au aya za Korani na hata aya za Bibilia katika kupamba kuta na milango na nyumba zao Mathalani Piga Hodi Mara Tatu Ukiona Kimya Ondoka Zako”
Mwanakwetu akakiomba hiko chungu ili siku akiwasimulia wanawe awe na ushdaahidi. Sasa Iddi Rangweni kumbuka anaendelea anafagilia makaburi sasa akaingia kaburi la Shabani Rangweni aliyefariki mwaka 2012 akafanya usafi anayatoa majani katikati akakutana na shimo limechimbwa jamaa akafukua kukawa kama pamezikwa kitu akafukua akakutana na bati dogo chakavu , akafukua akakutana kitu cheupe kimefungwa na kitambaa cheupe kikiwa kimeandikwa kwa maandishi mekundu, huku kukiwa na nyota zilizochorwa. Kumbuka huyu kijana mdogo tuliye naye analia anasema baba usishike baba usishike.
Mwanakwetu akaingilia kati akafungua kitambaa cheupe akaweka kando, kukiwa kimefungwa na kamba tatu juu, kati na mwisho. Kufungua ndani Mwanakwetu akakutana na toto la mkungu wa ndizi likiwa limefungwa na kuna vitambaa vyeusi, hilo likiendelea huku Mwanakwetu anapiga picha hatua kwa hatua.
Jamaa akawa anaendelea kufanya usafi wa makaburi hayo akaingia kaburi la Asia Rangweni hapo hakukutana na kitu akarudi kaburi lingine na hapa Iddi Rangweni akakutana na yai ambalo lilikuwa limeandikwa maandishi na kuchorwa kwa peni za rangi nyeusi na nyekundu.
Hapo Mwanakwetu anapiga picha hatua kwa hatua, haya matukio makaburini yalimshangaza mno Mwanakwetu.
Jua lilipopungua tukaondoka zetu kurudi nyumbani kwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mwanadilatu Kitindi Rangweni, mwendo mrefu kwa miguu, tulipofika hapo tu tukamsimulia tulivyotatua ule mgogoro wa mpaka na ndugu Rosana Marwa alafu yale tuliyoyaona katika makaburi ya ndugu zake.
KANISA KATOLIKI KIGANGO MWANADILATU
Kitindi akasema akasema,
“Hawa jamaa hawana adabu, hata mimi mwaka 2019 nilipita hapo makaburini nikakutana na kitambaa chaupe kimeandikwa majina ya wagombea wa serikali za mitaa jina ambalo halikuwepo nilitambua ndiye aliyefanya uchafu huo, nikakibeba hadi kwa mgombea nyumbani kwake nikakiweka barazani kwake huku nikimuadhibu kwa maneno makali, hapo hapo jamaa aliomba msamaha.”
Baada ya mazungumzo haya, Mwanakwetu alipanda gari na kurudi zake Mbagala.
MIONGONI MWA MISIKITI YA MWANADILATU
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mosi kwa sasa mwenye huitaji wa kutatua changamoto Serikali za Vijiji / Mitaa, tembeleeni mapema ofisi hizo kabla ya uchaguzi ili kuepusha hiyo migogoro kuhamia kwa uongozi mpya.
Shabaha ya pili kila mmoja amefiwa na ndugu na jamaa yake, jamani nawaombeni tembeleeni makaburi ya ndugu zenu mfanye usafi maana washirikina wanafanya mambo kipuuzi makaburini.
Mwisho kabisa Septemba 19, 2024 Mwanakwetu anatimiza miaka 50 hivyo makala haya yameandikwa hasa juu ya imani ushirikina makaburikin na maka hya kama zawai ya wasomaji wake kujifunza hilo kwa miaka 50 ya Mwanakwetu.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka,
“BABA USISHIKE
-USHIRIKINA MAKABURINI.”
Nakutakia Siku Njema.
NB Maana ya Jina MwANA DILA TUU-ni maneno ya Kizalamo yakimaanisha mtoto muache alie .
makwadeladius@ gmail.com
0717649257
Post a Comment