WATAPATIKANA KWELI AMA TUNAISHI MWITUNI

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Langoni Hodi Hodiii…

Mgeni Akiingia Mpokeee…

Mgeni Akiingia Mpokeee …

Mgeni Akiingia Mpokeee…

Makwega Akiingia Mpokeee…

Magogo Akiingia Mpokeee…

Mkombachepa akiiingia Mpokeee…

Msoka Akiingia Mpokeee…

Lushoto hodi hodi

Mgeni Akiingia Mpokeee…

NYIMBO ZA KISAMBAA-Liz Msoka Septemba 7, 2017.

Msomaji wangu huo ulikuwa wimbo wa ukaribisho wa Kisambaa kama ulivyonukuliwa na Mwanakwetu katika Kijiji cha Langoni, Kata ya Mnazi yenye Wapare, Wasamba. Wamasai, Wambugu na Wakamba katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Septemba 7, 2017 ambapo Mwanakwetu na wenzake kadhaa walifika hapo katika shughuli za Kiserikali.

Wimbo huu uliongozwa na Bi Elizabeth Msoka, mama mmoja wa Kichaga ambaye alikuwa Afisa Mifugo wa Wilaya hii katika ziara hiyo. Eizabeth Msoka aliajiliwa na Halmashauri ya Lushoto miaka mingi tangu akiwa binti mdogo, hivyo japokuwa alikuwa Mchaga aliweza kuwa sehemu ya makabila haya ya Lushoto huku akizungumza Kipare, Kisambaa na Kimbugu vizuri sana.

Kwa hakika Kwa bahati mbaya Mwanakwetu alipitiwa kumuuliza Bi Msoka, Je Lushoto ndipo alipopata mume? Kama Mwanakwetu akienda tena Lushoto, pale akipata nauli kwa hakika  atamuuliza huyu Bibi wa Kichaga swali hilo na ana hakika jibu lake msomaji wangu nitakujulsha.

Kwa hesabu za Mwanakwetu kwa mwaka huu wa 2024 anaamini Liz Msoka ameshastaafu akiwa mtumishi mmoja mchapa kazi ambaye Mwanakwetu alimuhusudu, alimtunuku na kumpenda sana sana.

Mkutano ulifanyika vizuri ambapo yalikuwa majira ya mchana kuelekea jioni huku shughuli kadhaa za maendeleo zilikaguliwa mathalan Ufugaji, Kilimo, Afya, Biashara na Elimu.


 

Baadaye msafara huo kufungasha virango na kuendelea na safari katika Tarafa hiyo ya Umba ambayo ulikuwa ni ukanda wa joto na jua kali, majira yake yakifanana fika na ukanda wa Pwani ya Tanzania wakati Lushoto ya Milimani ikiwa na baridi kali.

Tarafa ya Umba iliyo kando na Mto Umba unaopeleka maji ya yeke huo  nchini Kenya, wakati huo taraka hii iliongozwa na Afisa Tarafa aliyefahamika kama Mwalimu Moka, mzee mmoja makini na sasa mzee huyu ndiye Diwani wa Kata ya Lushoto.

Msafara huo uliondoka Langoni na kuelekea kama wanakwenda Lunguza na siku hii hakuna aliyekuwa anafahamu kuhusu wanapokwenda maana mtu mmoja tu ndiye aliyekuwa anafahamu hilo naye kama siyo Elizabeth Msoka basi ni Muhusini Magogo na kazi hiyo walikuwa wanapokezana. Huyu Muhusini Magogo alikuwa ni Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) sasa ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Shabaan Shekilindi-Lushoto Tanga.

Safari hii ilikuwa na kundi la watu wasiopungua 30 kwa hiyo watu wawili ndiyo waongozaji ili kulinda usalama wa watumishi hao. Mara zote Elzabeth Msoka au Muhusini Magogo walipanda katika gari la mbele wao ndiyo waongoza njia.

Ndani ya msafara huo walikuwapo pia wanahabari kadhaa akiwamo Herman Mbonea (Star TV& Radio Free Africa), Sofia Wakati(Uhuru & Mzalendo) Mashaka Mhando(Majira), Hellen Mushi (Utume FM) Wiliam Mgazija (ITV & Redio One Stereo), Joachim Kapembe na Bakari Katumbatu (TBC)

Wakiwa njiani gafla taarifa zilisambaa kuwa mhe. Tundu Antipas Lissu ambaye alikuwa mbunge wa Singida Mashariki amepigwa risasi huko Dodoma alipokuwa akitokea Bungeni kurudi nyumbani kwake nyakati za mchana.

Mwanakwetu alifungua simu yake na kutembelea ukurasa wa DW Kswahili na kukutana na habari iliyokuwa na maneno haya

“Mbunge Upinzani Tanzania Apigwa Risasi.”

Mwanakwetu aliisoma habari hiyo ambayo ilifanyiwa tafsiri na Mtangazaji Bruce Amani na kuhaririwa na Swaumu Mwasimba hawa wakiwa wanahabari wa kimataifa wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, huku wakiwa raia wenye asili ya Kenya, habari hii iliandikwa na Shirika la Habari la Ufarasa AFP.(AAAAFEEEPEEE)

“Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Mwigulu Nchemba anasema mwanasiasa huyo wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, alijeruhiwa na mshambuliaji asiyejulikana.

Nchemba anasema serikali itatoa taarifa baada ya kupata ripoti ya hali ya afya ya Lissu, ambaye pia ni Rais wa chama cha mawakili, Tanganyika Law Society. Lissu ni miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaoikemea na kuikosoa serikali. Mwanasiasa huyo amefanyiwa upasuaji wa dharura baada ya kupigwa risasi tumboni na watu wasiojulika nje ya nyumbani kwake mjini Dodoma.”

Mwanakwetu akawaambia hawa jamaa aliyokuwa nao, kumbe tukio hilo ni la kweli hadi AaaFeePee wameandika na DW Kiswahili wameitumia habari hiyo.

Mwanakwetu alijiuliza inakuwaje Mhariri Mkuu wa DW Kiswahili aliwapa watangazaji wenye asili ya Kenya kuifanya kazi hiyo? Kwanini ripoti hiyo hawakupewa kuitafsiri watangazaji wenye asili ya Tanzania? Haya alijiuliza moyoni tu akiamini kazi hiyo ingefanywa na wanahabari wenye asili ya Tanzania ingenoga zaidi.

Mwanakwetu akawa anaongea na wenzake ndani ya gari njiani akasema,

“Ukiona mtu maarufu anashambuliwa kwa risasi au kwa chochote tambua kuwa usalama wa mtu ambaye siyo maarufu upo katika hali mbaya zaidi, maana lolote au chochote chaweza kumkuta mtu wa kawaida na maneno  haya pia yalisemwa wakati wa hukumu kwa wale askari walihukumiwa baada ya kumpiga risasi kwa kumfananisha na jambazi Imrani Kombe ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa miaka ya tisini.”

Ndani ya gari hilo wakauliza kwani ilikuwaje tukio hilo la mauwaji ya Imani Kombe? Walijibiwa kuwa  Imrani Kombe alikuwa yeye na mkewe wanasafiri walipofika jirani na Moshi gari lake Toyota Hilux ilifananishwa na gari ya jambazi hivyo askari hao kutoka Kituo cha Polisi Osyterbay Dar es Salaam wakampiga risasi na kufariki.

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu na wenzake wanaendelea na safari na sasa wakafika Lunguza katika nyumba moja ya wageni inayofahamika kama MWAMBASHI naye Elizabeth Msoka akasema maneno haya,

“Mkuu siku ya leo tutakula chakula cha jioni hapa na kulala hapa na kesho tutaendelea na ziara.”

Kweli jioni hiyo kulifanyika kwanza tathimini ya ziara nzima ya siku hiyo, alafu kikaliwa chakula cha pamoja, mwisho ukawa utawala binafsi, watumishi wengi wakatazama taarifa ya habari alafu wakawa wanaongelea tukio hilo la mh. Tundu Lissu kupigwa risasi.

Mjadala ulikuwa mzuri sana ambapo mdau mmoja akasema unajua unaweza kupewa jukumu la kufanya jambo baya na ukaagizwa, hapa lazima ukatekeleze.

Mwingine akasema hapana, huyo anayekuagiza kwa nini hafanyi yeye mwenyewe?

Hata kama mtu ni mkosoji kiasi gani katika hii dunia hayupo mwenye mamlaka ya kusema huyo aondolewe uhai wake na ndiyo maana watu wanaofanya haya matukio wanafanya kwa siri, kama wao ni majasiri wafanye hadharani huku wakionekana sura zao.

“Waliofanya tukio hilo lazima watapatikane tu iwe leo, iwe kesho, iwe kesho kutwa na wataadhibiwa, nawaambieni duniani siyo mwituni.”

Kweli mjadala ulikuwa mkubwa na baadaye Mwanakwetu kwenda zake kulala na siku ya pili waliendelea na ziara hiyo .

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Kwa hakika maelezo ya mjadala huo kwa wafanyakazi wale katika  nyumba ya wageni ya Mwambasi ulionesha kuwa wapo watu wanaofanya matukio mabaya kwa kutumwa na watu waovu na anayetumwa anatekeleza tu kwa malipo au bakishishi fulani.

Katika mjadala ule wapo walioamini kuwa ipo siku watapatikana waliotekeleza jambo lile lakini tangu mwaka 2017 -2024 ni miaka zaidi ya saba ambapo mtoto aliyezaliwa 2017 sasa yupo darasa la pili na miaka inasonga .

Swali ni Je Waliofanya Tukio Hilo Watapatikana kweli ama Tunaishi Mwituni?

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka tu,

“Watapatikana Kweli Ama Tunaishi Mwituni.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

0/Post a Comment/Comments