NHIF JEMBE LISILO NA MAKALI LAKINI LINALIMA HATUA MOJA

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Mara zote Mwanakwetu amekuwa akisema kuwa alishuhudia baadhi ya watumishi wa umma ambao sasa wamestaafu wakati wakitoa maoni yao kwa wabunge wao juu ya kuundwa kwa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo kwa hakika watumihsi hao wa umma ambao wengine wamefariki na lakini wengine wapo hai huku wamestaafu, shaka zao ya wakati huu, ambapo Mwanakwetu  alikuwa kijana sasa ameamini kuwa mashaka ya ndugu yale yalikuwa sahihi.

Mwanakwetu anakumbuka kisa hiki,

“Ulikuwa mkutano wa kampeni za CCM baada ya jina lililopitishwa na CCM la ubunge kwa jimbo la Kasulu kufariki katika ajali ya gari . CCM waliketi upya na kumchagua marehemu Francis Musati ili wana wa Kasulu wapate kiongozi wao. Hapo hapo alipitishwa marehemu Francis Musati alifika Makere ambapo ndipo kijiji alichozaliwa kuanza kampeni. NCCR Mageuzi wakimsimamisha Francis Nzasikwago. Francis Musati siku hiyo iliyokuwa Jumapili asubuhi kwanza alisali Kanisa Katoliki la Makere. Hapo Kanisani Mwanakwetu alisali pia na baadaye kufanyika mkutano mkubwa wa kampeni za CCM stend ya Mabasi ya Makere jirani na msufi mmoja mkubwa.

Mwalimu Daudi Ruhinda na Mwalimu Rajabu Hussein walihoji juu ya NHIF kwa marehemu Francis Musati ambaye alikuwa mwanasheria kwa taaluma akasema , ‘Hilo nitalifanyia kazi , lakini jukumu lenu ndugu zangu, watu wa Makere ni kunipigia kura tu.’ Mwisho wa siku Francis Musati alishinda na kuwa mbunge wa Kasulu.”

Wakati wa kuanzishwa kwa NHIF yalisemwa mengi na walioshika vipaza sauti walitoa sifa tele sasa wamekaa kimya pengine hawana nafasi hizo tena, hiyo sasa ni karibu miaka 24. Huu ni umri wa kijana mwenye familia.

“Huu mfuko utakuwa mkombozi wa matibabu ya wafanyakazi.”

Waungaji mkono ambapo walikuwa na nafasi, wakilinda nafasi zao walisema, huku sasa wajukuu zao sasa wanapata tabu.

Miaka minne baadaye yaani 2004, Mwanakwetu akaingia Utumishi wa Umma na mwaka 2005 akawa mwanachama wa NHIF bila ya kujaz fomu mshahara wake wa shilingi 100,800/-ulikatwa pesa za mfuko huo.



Mwaka huu 2023 Bunge la Jamhuri ya Muungano la Tanzania limepitisha hoja /muswada wa wa Bima ya Afya Kwa wote, hilo mwanakawetu hana shaka nalo. Kinachofanyika ni kupitisha yatayokuwa yanaaminika yatatoa muelekeo wa matibabu hayo kwa  wote.

Mwanakwetu anaamini kuwa jina la Bima ya Afya kwa Wote lenyewe lina maana na kuwavutia wengi kuwa sasa ni mkombozi wa Watanzania wote lakini kuna maswali mengi ya kujiuliza,

“Je matumaini hayo kwa watu wote yanaweza kufikiwa kweli na Watanzania wote wakatibiwa kila ugonjwa walio nao kama ilivyokuwa nyakati za UJAMAA? Kama matumaini ya Bima ya Afya ya NHIF yakiwa bado yanajikokoja kwa kundi dogo, vipi kwa kundi kubwa kama hilo?Au tunataka tuanze na jina zuri alafu baada ya miaka mitano kelele kila kona alafu watu watasema.’ Jamani nchi hii kubwa, ina watu wengi , suala la afya ni gumu jamani kila mmoja ajitibie mwenyewe !’ ”

Mwanakwetu leo hii anaamini kuwa ,

“Kwa uzoefu wangu mdogo wa mwaka 1999 na 2000 ninapata picha ya NHIF kama jembe lisilo na makali , huku sasa dhana ya Bima ya Afya Kwa Wote naiona kuwa ni Jembe lenye makali ambalo lipo dukani, wakati hata huyu mkulima hana uwezo wa kulipata, lakini mkulima huyu amejazwa na matumaini kuwa sasa atapata jembe lenye makali.”

Mwanakwetu anaamini kuwa NHIF hata kama ni jembe lisilo na makali lakini linaweza kulima hata hatua moja, dhana ya kujenga matumaini makubwa kwa jembe linalodhaniwa kuwa lina makali ambapo lipo dukani siyo dhana sahihi.

Mwanakwetu anashauri kuwa hili Jembe Lisilo na Makali libaki likilima hata hiyo hatua moja kidogo kidogo, nalo hilo Jembe Lenye Makali wakati mipango yake ikikamilika mkulima apewe na lianze kazi. Mipango ikamilike. Huko kusaini sheria na vikao haina maana yoyote kwa Mtanzania mgonjwa.

Dhana ya Bima ya Afya Kwa Wote isitumike kuupiga shoka na kuuuwa mfuko wa NHIF, hilo ni kosa kubwa ambalo pengine baadhi ya wajanja wanaweza kutumia kuficha madhaifu ya NHIF na madhaifu ya utendaji .

Mwanakwetu anapata picha hii,

“Kumbe NHIF ilikuwa ikifanya uwekezaji mkubwa wa majengo makubwa makubwa ili kuweka misingi kwa BIMA YA AFYA KWA WOTE? Wanachama wake wanapata tabu, wanasumbuliwa kumbe kuna kitu mbele yake! Nimetembelea tovuti ya NHIF sasa imeanza kutumiwa kupachika habari za BIMA YA AFYA KWA WOTE. Hilo ni suala la Wizara ya Afya na siyo la NHIF“

Mfuko NHIF uendelee , pesa zake , rasilimali zake, mtaji wake , majengo yake na wanachama wake, watumishi wake waendelee na na mfuko wao huku BIMA Y AFYA KWA WOTE ianze kazi kwa kila kitu kipya na rasilimali zake mpya.



Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Isije ikafika mwaka 2050 kwa wale watakao bahati kuwa hai, mfuko huu wa Bima y Afya Kwa Wote umekufa.

Kikubwa siyo kuundwa kwa taasisi au kubadilisha majina, kikubwa Watanzania watibiwe bure ili waweze kuendesha maisha yao na waweze kushiriki vizuri katika shughuli za maendeleo kama ilivyokuwa wakati wa UJAMAA.

Mwanakwetu Upo?

Jembe la Zamani na Jembe Jipya yote yabaki shambani yafanye kazi na kila jembe na ngwe yake.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmaill.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments