Msomaji wa matini hii nakukumbusha kuwa katika sehemu ya pili
nilikueleza namna Wapare walivyofanya utani katika sherehe zao za tohara za
wasichana na wavulana na namna walivyokuwa wakiimba katika sherehe hizo.
Leo naendelea na namna maisha ya vijana wa kike na wakiume
walivyokuwa wakiishi katika jamii ya Wapare. Mabinti na wavulana ambao walikuwa
wamepevuka walikuwa wakiishi katika nyumba maalumu ambayo ilikuwa inafahamika
kama BWENI.
Neno hilo BWENI lina asili ya kabila hilo la Wapare likimaanisha
nyumba wanayokaa vijana wa rika hilo. Nyumba hiyo ndipo vijana wengi walipata
wachumba wa kuoana na kuishi pamoja. Hapo palikuwa ni pahala ambapo vijana
hukaa na kutaniana na kubadilishana mawazo.
Katika nyumba hiyo ngoma huandaliwa kwa sherehe kadhaa ambapo
zana za muziki kama malimba hupigwa. Katika shughuli hiyo ndipo vijana hujaribu
kueleza hisia zao kama kumkubalia mtu au kumkataa. Hapo nyimbo huimbwa katika
mitindo ya mashairi yenye ujumbe wa sifa kwa wapenzi, tabia njema na kadhalika.
Wapare pia wana neno lingine linalofahamika kama KINJI, hiki ni
kitendo cha kwenda shambani kulinda mazao yaliyokomaa hapo huwa ni wakati wa
kulinda mazao hayo ili yavunwe yakiwa salama.
Wakiwa katika malindo hayo hata wakati wa usiku wengine hupanda
juu ya mawe huku wakiimba au kuzungumza na wenzao walio katika mashamba mengine
kwani sauti husika viizuri sana muda huo. Wakati zoezi hilo la kulinda mazao na
wanyama waharibifu likifanyika vijana hao ukoka moto na kuzungumza mambo kadhaa.
Wapare wanao utani katika ndoa lengo nikuongeza ujirani baina
yule anayetaniwa na mwenzake.
Ndugu F.A. Mzava ambaye naye ni Mpare katika mojawapo ya kazi
zake za utafiti kwa kbaila hili anasema kuwa watani wakubwa wa Wapare ni
Wachaga na Wasambaa na jambo hilo linashangaza kuwa Wapare kwa mtu ambaye siyo
wa kabila lao humuita MNYAMWEZI lakini Wasambaa na Wachaga kwa Wapare hawaitwi
WANYAMWEZI.
Ndugu Mzava anadai kuwa ujirani huo ambao unakuwa sawana na
udugu ulivyoimarishwa na ule utani baina yao.
Ndugu Mzava anasema kuwa kuna wakati akiwa kwao Upareni
alisimuliwa habari ya ndugu mmoja aliyekuwa na kaka yake na baba yake. Baba yao
aliamua siku moja waende kumtembea rafiki yake aliyekuwa jirani na kijiji chao.
Kaka huyo aliyemsimulia Ndugu Mzava waliianza safari hadi huko .
Walipofika kwa rafiki wa baba yao walipokelewa. Rafiki wa mzee huyo alimuuliza
baba wa hawa vijana:
“Uyoa ni naio ngese nyose.”
Mwenyeji huyo alimaanisha kuwa unakwenda wapi na watu wote hao.
Jambo hili liliwaumiza mno vijana hawa, lakini baba yao aliona ni jambo la
kawaida tu, akitambua hicho kilichofanyika ni utani.
Kiukweli kabisa jambo hili linaweza kumsababisha yule alikwenda
kumtembelea rafiki yake kugeuza na kurudi alipotoka lakini hilo halikufanyika
hivyo.
Kuna mfano mwingine kuwa ndugu mmoja alikuwa amesafiri muda
mrefu sana na siku hiyo alikuwa akirudi kutoka safari, mara alipita kwa rafiki
yake kumsalimia, ndugu huyo alimuuliza eh unatoka wapi? Jamaa aljibiwa kuwa
yeye anatoka safarini. Jirani akasema kumbe hautoki nyumbani kwako? Jamaa
alijibu ndiyo.
“Tumanyije
iti mwana wako afwa.”
Jamaa akamwambia kuwa kwako kuna msiba mwanao amefariki. Kwa
kuwa walikuwa watani jamaa huyu hakumtilia maanani alikaa kimya hapo na kunywa
zake maji na kuondoka zake
Katika kumalizia kabila hili kumekuwa na maswali ya Imani ya
Wapare katika ushirikina.Je Wapare wanaamini katika uchawi? Kulijibu swali hilo
F.A. Mzava anasema kuwa;
“Wapare wanaamini katika ushirikina lakini wanaamini kuwa mtani
hawezi kumroga mtani mwenzake na ndiyo maana ilikuwa vigumu mno kumsikia Mpare,
Msambaa na Mchaga juu tuhuma hizo wakati huo. Ndiyo kusema kila wakati mtani
humtakia mema mtani wake.”
Mwanakwetu kwa leo naiweka kalamu yangu chini, nikihitimisha
safari ya kabila hili la Wapare na utani ndani yake. Nina hakika kwa kiasi
umetambua namna Wapare wanavyofanya utani na watani wao Wasambaa na Wachaga.
Katika matini ijayo nitalitazama kabila la Wangindo, Je Ungidoni
kuna nini? Subiri matini ijayo.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment