ABIRIA MWENYE BEGI KUBWA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Shajara ya Mwanakwetu ya Agosti 2023 inasimulia kuwa Mwanakwetu alikuwa njiani akisafiri kutoka Dodoma kuelekea Mwanza, alipofika stendi ya Nanenane Dodoma alikuwa na begi moja kubwa ambalo wakati linapakiwa dada utingo na kondakta wa basi alilopanda alisema,

“Kama kaka mwenye begi kubwa unashuka Mabuki , hapo ni njiani , haufiki Mwanza Mjini, hivyo begi lako linatakiwa kukaa upande wa mlango na jirani,  kwa hiyo nisubiri hapo alafu nitaliweka baada ya kuliwekea alama ya mwenye begi.”

Kondakta wa basi hili alikuwa binti mwenye siha nzuri tu na ana nguvu , wala hakuhitaji msaada wa mtu yoyote kupanga mabegi na masanduku hayo ya abiria.

Zikiwa zimebakia kama dakika tano, binti huyu akasema,

“Kaka mwenye begi kubwa , njoo naomba nitajie namba ya kiti yako “

Mwanakwetu akataja 43 na dada huyu akapakia begi na kuandika namba 43 kwa kirumi XLIII kwenye karatasi nyeupe iliyopachikwa katika begi hilo, naye Mwanakwetu kuingia ndani ya basi hilo la Dodoma Mwanza.

Wakiwa ndani akatokea abiria mwingine na mizigo mingi, kondakta akaingia ndani ya basi akasema,

“Yule kaka mwenye begi, kaka mrefu yupo wapi? Nakuomba kidogo maana nahamisha mzigo wako, uje uone ninapouweka na nakuomba usikae kiti namba 43, kipo kiti kingine maalumu kwako wewe, abiria wangu mwenye begi kubwa.”

Mwanakwetu alishuka na kwenda chini ya basi na begi lake likatolewa na kuwekwa mabegi na masanduku kadhaa, alafu begi la Mwanakwetu likapelekwa katika chumba cha buti kingine mbele ya mlango wa mbele wa abria maana basi hili lilikuwa na milango miwili ya kushuka na kupanda abiria.

Begi hilo likaandikwa nambari XLVI naye Mwanakwetu akaambiwa akakae kiti hicho huko nyuma kabisa ya basi hilo.

Kiti hicho kilikuwa na nambari 45 na 46 ziliandikwa kwa namba za Kiarabu, Mwanakwetu hapo alimkuta binti mmoja amekaa. Safari ikawa inaendelea vizuri mno, huyu kondakta wa kike alikuwa akizunguka mara akikagua tiketi , mara akipokea pesa na mara akitoa vinywaji na vitafunwa kwa abiria wake.

Kila kondakta huyu wa kike akifika alipokaa Mwanakwetu neno la uchokozi lilimtoka na kumtania Mwanakwetu , hapo Mwanakwetu alibaini kuwa binti huyu alikuwa mtundu sana tangu  alipokuwa mdogo.

Abiria mwenye begi kubwa sijakupa pipi yako eeh.

Abiria mwenye begi kubwa soda yako hii hapa

Abiria mwenye begi kubwa anakunywa pepsi!

Utani huo wa kondakta huyu ulisababisha abiria binti kando ya Mwanakwetu ashangae mbona kondakta huyu hana soni na ana nini na huyu abiria mwenye begi kubwa? Binti huyu akauliza unamfahamu huyu  kondakta? Mwanakwetu alijibu hapana.

Utani huo wa kondakta kwa abiria mwenye begi kubwa na swali la dada abiria kando uliibua maelewano makubwa baina ya Mwanakwetu na huyu abiria mwenzake. Binti huyu bila hiana alimjibu Mwanakwetu kila swali alilouliza likiwamo namba ya simu, jina na kazi anayofanya.

“Mimi ni mwanachuo wa chuo cha Diplomasia Kurasini na nipo njiani kwenda nyumbani kuna msiba wa mjomba .”

Kumbe unasoma Diplomasia Kurasini !

Je unamfahamu Dkt Jacob Nduye?


(Dkt Nduye)

Mwanakwetu aliuliza.

Binti huyu alijibu kuwa anamfahamu ni mhadhiri wao, Binti huyu alifurahi mno abiria mwenye begi kubwa kumfahamu Dkt Nduye , alafu akamuuliza wewe unamjulia wapi Dkt Nduye? Au alikusomesha.

“Yule ni kaka yangu kabisa, tunatoka wote kwetu Morogoro sisi ni vitukuu wa Chifu Morogoro .”

Binti huyu akamuuliza swali lingine, abiria mwenye begi kubwa jina lake halisi unaitwa nani? Mwanakwetu alijibu kwa kumpwaga  

“Mimi naitwa Melkizadeki Nduye aka Kuhani Mkuu.”

Binti akawa anacheka sana, alafu akauliza mbona , mbona nyinyi wachangamfu sana ? Hata Dkt Nduye ni mchangamfu sana kama wewe .

“Sisi tunazaliwa katika ukoo wa chifu Morogoro, sisi hiyo Morogoro mali yetu, hivyo ukoo wa machifu mnapokea wageni wengi, kila siku kwa hiyo lazima uwe chakalamu na siyo mnyonge mnyonge.”

Binti anacheka, mara kondakta anakuja anasema ahaaa kaka mwenye begi kubwa unanikwepa au umeshapata mwingine?



Mwanakwetu hakusema neno alikaa kimya tu.

Baadaye Mwanakwetu akamwambia ukweli binti huyu kuwa Dkt  Jacob Nduye alifanya naye kazi TBC Taifa akiwa ni mtangazaji na mtayarishaji mzuri sana wa vipindi vya redio .

Binti akauliza ni kweli alikuwa akitangaza eeeh? Mwanakwetu akajibu ndiyo na vipindi vyake vilikuwa Mtaalamu na Wetu, Biashara na Uwezeshaji na hata mada za kuwahoji viongozi na kazi hiyo aliifanya vizuri sana.

Binti huyu akauliza swali lingine eeeh kwani alikuwa anapenda nyimbo gani?

“Mimi nimefika TBC Taifa nilimkuta Seleiman Muhogora , Malima Ndelema, Abisai Stephern ,Abdul–Rahamin Nzota, Sued Mwihyi hawa ndiyo walikuwa watayarishaji vipindi na watangazaji wakiume kidogo wakubwa na wale wenye umri wa kati alikuwepo Dominiki Mrikoni , Benedict Komba , Alex Magwiza na Jacob Nduye.”

Binti akasema naomba nitajie nyimbo alizokuwa akizipenda kucheza akiwa studio.

“Nduye alipokuwa zamu studioni alizipenda nyimbo mbili ya kwanza ni Samahani ya Uwongo.”

Nilidhani kwamba utanisaidia katika matatizo ya dunia,

 Kumbe uwongo

Ukiwa kama rafiki yangu mpenzi wa jufa na kuzikana duniani,

Kumbe uwongo

Matokeo yake, huna hata aibu ,unaniomba samahani

Kumbe uwongo

Binti huyu akawa anaandika jina la wimbo huo na baadhi ya mashairi yake kwa ufupi katika simu yake ya kiganjani.


(Tancut Almas)

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo safarini akitoka Dodoma kwenda Mwanza na anashuka Mabuki.

Binti huyu aliomba atajiwe wimbo mwingine aliyokuwa akiupenda na kuucheza sana Dkt Jacob Nduye akiwa studio za TBC Taifa.

Ninakwenda safari, safari yenyewe safari ya kikazi

Najua hapa utabaki watasema mengi

Pia wabaya wetu mama watafurahi

Lakini usisikie ya hao mama watoto

Ninakwenda kutafuta maisha ya watoto wetu

Chunga watoto, mama nitarudi, tutaonana kwa mapenzi ya Mungu

Chunga watoto mama nitarudi , Tutaonana kwa mapenzi ya Mungu

Safari siyo kifo mama yelele

Subiri nitarudi mama watoto

Nikirudi mama nitakuletea zawadi, zawadi mama watoto

Nikirudi mama nipokee kwa mikono miwli,

Huyu mwamafuzni alikuwa anafurahia hasa ujumbe wa nyimbo hizo ambazo zilizokuwa zinachezwa na Dkt Nduye akiwa mtangazaji ambapo Mwanakwetu alimshuhudia , hizo zikiwa nyimbo zilizoimbwa na Tancut Almasi ya Iringa Tanzania , Huku huu wimbo wa mwisho unaitwa Masafa Marefu.

Msomaji wangu safari inaendelea na  Mwanakwetu alibaini kitu,

“Dkt Jacob Nduye anakaa vizuri na wanachuo hao na kama anafundisha basi anatoa alama za masomo kwa haki.”

Kama angekuwa ana shida mhadhiri huyu binti huyu asingevutiwa kabisa na habari za msomi huyu zilizosimuliwa na Mwanakwetu..

Hapo safari iliendelea na Mwanakwetu akapitiwa na usingizi kwamuda mrefu lakini baadaye akamsikia kondakta akimuamsha huku akimuita ,

“Kaka mwenye begi kubwa, kaka mwenye begi kubwa basi limefika Mabuki shuka shuka kaka.”

Mwanakwetu alikurupuka usingizini na kushuka basini, nalo begi lake kushushwa na kungoja mabasi ya safari ya Malya Kwimba mkoani Mwanza.

Mwanakwteu Upo ?

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

 

 

0/Post a Comment/Comments