VIJANA WAWILI

 


 VIJANA WAWILI

Adeladius Makwega-Buigiri

Majuma matatu yaliyopita ndugu mmoja wa mwanakwetu alikuwa nyumbani kwake huku akitekeleza majukumu ya hapa na pale, gafla akasikia hodi nyumbani hapo. Hodi hiyo iliitikiwa na hapo mlangoni alikuwa mgeni akibisha. Kijana mmoja mrefu, mwembamba ambaye alikuwa mwanachuo wa chuo kimojawapo, alisalimia huku akipepesuka, akaegemea ukuta wa kiwambaza cha nyumba hii.

“Jamani mnanifahamu?”

Alijibiwa kuwa hawamfahamu kabisa kijana huyu.

Kijana huyu alisema kuwa yeye anawafahamu vizuri na ndiyo maana amefika hapo nyumbani ana shida.

Alijitambulisha kwa kina ndipo alifahamika na kukaribisha sebuleni kuketi. Kijana huyu alisema kuwa yeye ni mwanachuo amefika hapo kuomba msaada wa chakula hajakula kwa siku zaidi ya tatu, hivyo aliona kuwa si vizuri akafa kwa njaa wakati anaona uwezo wake wa kuwafuata binadamu wenzake anao.

Nduguze mwanakwetu walipomtazama walibaini kuwa ni kweli sura ya kijana huyo alionekana hajala chakula kwa siku kadhaa, macho yakiwa yememuingia ndani hata kuyafungua ilikuwa kazi kubwa.

Akaulizwa uwepo wake hapo masomo karo na huduma zingine analipiwa na nani?

“Ninalipiwa na mama yangu mzazi ambaye ni mfanyabiashara wa sokoni huko Mara na baba yangu mzazi alishafariki muda mrefu, mama ndiye kila kitu.”

Kweli kijana huyu kwanza alipewa chakula akala alafu akapewa shilingi 6000/ na kijana huyu aliondoka zake kurudi chuoni kuendelea na masomo.

Mkaa bure si mtembea bure, mama wa kijana huyu huko Mara alipata pesa na kumtumia kijana wake na hiyo ilimsaidia akaendelea na masomo, akafanya mitihani na alipomaliza mitihani yake alipita kwa nduguze mwanakwetu akaaga na kurudi zake Mkoani Mara.

Baadaye mwanakwetu akasimuliwa kisa hiki kusimulia kisa hicho alisikitika sana.Akilini mwake alikifananisha kisa cha kijana huyu na tukio la mwaka 2019/2020 la kijana mwingine kwa kiume ambaye alikuwa masomoni.

Wakati huo wanachuo wakijiandaa na mitihani ya ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada kulikuwa na kijana mmoja mdogo mwenye akili sana maandalizi ya mitihani yanaendelea huku kila mwanachuo akitakiwa kuingia chumba cha mitihani akiwa amelipa karo.

Jina la kijana huyu lilionekana kwa wasiolipa karo kwa hivyo alimtafuta nduguye mwanakwetu kuomba msaada wa mawazo katika kipindi hicho kigumu.

Ndugu wa mwanakwetu alimpokea kijana huyu kwa upole na kumuuliza nani ni mlipaji wa karo yake?

“Baba yangu ambaye alikuwa ni mtumishi wa umma huko Mkoani Morogoro amekamatwa kwa makosa ya hujuma za uchumi katika wilaya moja inayopakana na Lindi.”

Nduguye mwanakwetu kwanza aliogopa kumsikiliza kijana huyu, kesi ya Kuhujumu Uchumi? Baadaye roho ya imani ilimjia na kumuuliza kazi ya baba wa huyu kijana ilikuwa ipi?

“Baba yangu alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri, mbunge wake alimlalamikia, aliondolewa Ukurugenzi akahamishiwa TAMISEMI–Dodoma ndipo baadaye akakamatwa na kuwekwa ndani, uchunguzi na kesi unafanyika amepelekwa mahakaman ndiyo maana sasa sijaweza kulipiwa karo ya chuo.”

Nduguye mwanakwetu alimuuliza kijana huyu kama wanamiliki mali yoyote? Kijana huyu aliijibu kuwa hawana chochote na kama wangekuwa na mali basi karo ya shilingi 700,000/- kwa muhula isingekuwa tatizo na huku mama yake mzazi akiwa mama wa nyumbani na Dodoma wakiwa wanaishi katika nyumba ya kupanga.

Ndugu wa mwanakwetu alipoambiwa hivyo aliwasaliana na nduguye mwingine kuhakikisha kama yaliyomfika kijana huyu yalikuwa ya kweli, alibaini kuwa yalikuwa ni kweli kabisa.

Baadaye kijana huyu aliekezwa kuchukua fomu maalumu ya kujaza ili kuweza kupata msaada ili kumruhusu afanye mitihani hiyo. Kijana huyu baada ya siku moja alikata tamaa akafungasha vitu vyake na kuondoka chuoni hakupatikana tena hadi kesho

Kumbuka katika maisha kila jambo lina mwanzo na mwisho wake liwe baya liwe zuri mwanakwetu lina mwisho, shauri liliendelea na tamati baba wa kijana huyu hakuwa na hatia yoyote ile lakini kijana wake alishakosa masomo ya chuo hicho je alikwenda kuendesha bodaboda au kufanya kazi gani, Mungu anafahamu hilo, kweli kila binadamu ameumbiwa mitihani.

 Je siku ya leo mwanakwetu anasema nini?

Msomaji wangu pata picha ya vijana hao wawili huyu mwenye asili ya Mara na huyu ambaye baba yake aliyekuwa na shauri mahakamani, wanashindwa kusoma vizuri wa kwanza baba yake ni marehemu wa pili baba yake alikuwa kolokoloni, hapo jaribu kuvaa viatu vyao kuwa vijana hawa wawili ni wa kwako wewe unayesoma matini haya unajisikiaje?

Mimi na wewe ni wazazi, haya ynaweza kumkuta mwanao, mjukuu wako au hata kitukuu chako. Sasa tunafanya nini? Tunapaswa kuwa makini sana kwa malezi ya watoto wetu katika mambo ya umma pengine mifumo yetu inaweza kuwa chanzo cha matatizo hayo kwa kujua au kutokufahamu.

Taasisi za elimu zote za umma zinapaswa kutambua kuwa zenyewe zinatoa huduma kwa jamii ambayo ndiyo wenye mali, hawa Watanzania. Wanachuo wenye shida kama hizo wasikilizwe vizuri mambo ya kufukuzana kwa hoja ya karo si jambo la kiungwa na, msamiati wa kufukuzwa kwa kukosa ada kwenye taasisi za umma unapaswa kufutwa mara moja.Swali la kujiuliza wanaosimamia taasisi za umma kama mwanachuo aliacha chuo je shida ilikuwa ni nini?Je chuo kilichukua hatua gani kulitatua hilo? Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali anaweza kuhoji hilo.Kwa kufanya hivyo tunaweza kulinda watoto wengi wa Kitanzania wanaopatwa na kadhia hiyo.

Pia Mahakama inapoendesha mashauri yoyote dhidi ya mtu yoyote kwa kesi yoyote inapaswa kutambua kuwa mtuhumiwa huyu ni mzazi kama alivyo Jaji, Hakimu, Mwendesha Mashitaka, Polisi, Karani wa Mahakama, watuhumiwa hao waulizwe je familia zao zinaendeleaje wakati shauri hilo linaendelea maana mtuhumiwa anaweza kuwa amechanganyikiwa na hakumbuki lolote juu ya masuala ya msingi ya watoto wake.

Mifumo ya kiserikali ifahamu kuwa watoto hawa ndiyo Watanzania hao hao, wanapoona wamepunjwa chochote kutokana na sababu yoyote ile inaleta tafsiri mbaya ndani ya fikra zao na kujenga taifa lenye mambo mengi mioyoni mwao

Mwanakwetu upo?

Nakutakia Kwaresma Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

(NB Picha zote tatu ni za maktaba siyo wahusika wa visa hivyo)

0/Post a Comment/Comments