Adeladius Makwega – Musoma, Mara
Katika maisha ya mwanadamu, kila mmoja hutafuta riziki yake ili aweze kujikimu yeye mwenyewe na familia yake.
Hali huwa ngumu zaidi kwa vijana, kwani wao ndiyo huanza maisha ya kujitegemea huku wazee walioishiwa nguvu, wagonjwa na watoto wakitegemea msaada wao ili kuyaweka mambo sawa.
Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya idadi ya watu yaliyotokana na data za Umoja wa Mataifa (UN), idadi ya watu wa Tanzania mwaka 2026 inakadiriwa kuwa takribani milioni 72.6. Muundo wa umri wa wananchi wa taifa hili unaonyesha kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana.
“Umri wa miaka 0 hadi 14 ni watu milioni 30.58, sawa na asilimia 42.15 ya idadi ya watu. Hawa ni watoto na vijana. Umri wa miaka 15 hadi 64 ni watu milioni 39.78, sawa na asilimia 54.82; hawa ndiyo nguvu kazi ya taifa. Watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi ni milioni 2.2, sawa na asilimia 3.04 ya idadi ya watu.”
Takwimu hizi zinagonga kengele ya hatari kuwa zaidi ya watu 4 kati ya 10 nchini Tanzania ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15, huku takribani asilimia 3 tu ya wananchi wakiwa na umri wa miaka 65 au zaidi. Hali hii inaonyesha kuwa Tanzania ina muundo wa idadi ya watu vijana wengi, jambo linaloweza kuwa fursa kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ikiwa vijana watapata elimu, ujuzi na ajira zinazostahili na kama watatumika vizuri.
Kazi ambazo kijana anaweza kufanya zinaweza kuwa katika ajira rasmi au sekta binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, mwishoni mwa mwezi Mei na mwanzoni mwa Juni 2026, ilipokea watumishi kadhaa wa ajira mpya katika Kitengo cha Fedha na Uhasibu.
Jambo hili lilimvutia mno Mwanakwetu, akisema:
“Kumbe hapa kwetu vijana wamepata ajira.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wafanyakazi hao walionekana wakitekeleza majukumu yao ipasavyo huku wakiingizwa katika mifumo ya mahudhurio, barua pepe za Serikali na mfumo wa tathmini za utendaji kazi.
“Jamani samahanini sana, mimi ni ajira mpya, naomba nifunguliwe barua pepe ya Serikali.”
Haya yalikuwa maelezo ya Abdulrahman Hemed Said, mhasibu wa ajira mpya, akijitambulisha mbele ya Afisa TEHAMA wa Mkoa wa Mara, Switbert Sigsbert Masumira, ili aingizwe katika mifumo hiyo.
Ndugu Abdulrahman Hemed Said ni mhitimu wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM). Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja Katika ya jiji la Dar es Salaam, huku elimu ya sekondari akiipata katika Shule ya Sekondari Mvono.
“Nimefika Musoma, mkoani Mara, kwa mara ya kwanza. Nina furaha kubwa kufanya kazi kandokando ya Ziwa Victoria; nahisi kama nipo jirani na Bahari ya Hindi huko kwetu Pwani. Kwa hakika nimeyapenda mazingira haya. Ninaungama wazi kuwa nimekuja kuwahudumia vizuri wananchi wa Mkoa wa Mara ambao ni Watanzania wezangu”
Ndugu Said alisema.
Ajira hizo mpya hazikutolewa kwa wanaume pekee, bali hata kwa wanawake. Mwanakwetu alikutana pia na Agnes Christopher Kimwaga.
Mwanakwetu alimuuliza:
“Wewe ni kabila gani?”
Bi. Kimwaga alijibu kuwa yeye ni Muha. Mwanakwetu akamsalimu:
“Ulokomeye(Haujamb).”
Bi. Kimwaga alicheka huku akisema:
“Sasa nipo jirani na Mkoa wa Kigoma. Kiha sikifahamu vizuri, lakini itabidi nijifunze ili niifahamu lugha ya kwetu, maana Mkoa wa Mara upo jirani na Mkoa wa Kigoma.”
Bi. Agnes Christopher Kimwaga ni mhitimu wa Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM). Elimu yake ya sekondari aliipata katika Shule ya Sekondari Eden na Shule ya Wasichana ya Weruweru.
Katika pita pita zake, Mwanakwetu alikutana pia na Bi. Husna Sudi Nassoro, ambaye alijitambulisha kuwa ni mhasibu wa ajira mpya.
“Nimefika Mkoa wa Mara. Kabla sijaja nilikuwa na picha tofauti kabisa kuhusu mkoa huu, lakini sasa nimeuelewa. Kumbe ile picha niliyokuwa nayo haikuwa sahihi. Nimeanza kazi vizuri, nimepokelewa vizuri na nina amani pamoja na furaha tele.”
Mapema Juni 4, 2026, macho ya Mwanakwetu yalikutana na tabasamu murua la Bi. Flavia Stephano.
“Mama, na wewe ni mgeni hapa ofisini kwetu?”
Bi. Flavia Stephano alijibu:
“Ndiyo, mimi ni mgeni. Natokea jijini Dar es Salaam, ni ajira mpya. Kwa asili natoka Mkoa wa Kagera. Mimi ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nimeajiriwa kama mhasibu.”
Bi. Flavia Stephano alisema kuwa japokuwa kwa asili anatoka Mkoa wa Kagera, hajawahi kufika Mkoa wa Mara kabla ya kuajiriwa.
“Ninashukuru kupata kazi serikalini na kufanya kazi jirani na Mkoa wa Kagera. Nitajitahidi kutumia kila likizo kwenda nyumbani ili nile sesene na pia kuondokana na lawama za kutowatembelea ndugu, jamaa na marafiki.”
Kwa hakika, katika miezi ya Mei na Juni 2026, Mwanakwetu alikutana na ndugu hawa na kuongeza watu wapya katika orodha yake ya marafiki na watu anaofanya nao kazi.
Kwa hakika, Flavia Binti Stephano, Husna Sudi Binti Nassoro, Agnes Christopher Binti Kimwaga na Abdulrahman Hemed Bini Said ni miongoni mwa vijana walioajiriwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Mei mwaka 2026.
Mwanakwetu Anasema Nini Leo?
Kwa hakika, Tanzania ina idadi kubwa ya vijana. Hivyo basi, unapoona vijana wanapata mitaji au ajira mpya, tambua kuwa jambo hilo linaleta nafuu kubwa kwa jamii husika.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Ajira Mpya kwa Vijana Zinaleta Nafuu kwa Jamii.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)







Post a Comment