.gif)
Adeladius Makwega-Musoma.
Unapofika mkoani Mara unakaribishwa na mandhari nzuri ya maji yanayotiririka kuelekea Ziwa Victoria ndani ya Mto Mara unaanzia Kenya na kufika Tanzania na kulisalimu ziwa hili lenye utajiri mkubwa wa Samaki kama vile Sangara na Sato. Nalo Ziwa Victoria linauzunguka mkoa wa Mara mithili ya mtoto ndani ya tumbo la mama mjamzito.
Huku msomaji wangu ukumbuke kuwa Mkoa wa Mara ni moja ya mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Kaskazini mwa taifa hili la Afrika ya Mashariki na Kati ukiwa na KM za Mraba 20,150 wenyeji wakisema jina MARA likitokana na ule Mto Mara.
Kulingana takwimu ya idadi ya watu nchini Tanzania zinadokeza kuwa Mkoa wa Mara unashika namba 10 ya idadi ya watu wengi nchini Tanzania, ukiwa na watu 2,371,015 wanaume ni 1,139,511 na wanawake 1,232,504. Huku takwimu hizi zikidokeza kuwa kati ya watu hao nguvu kazi ni asilimia 48.3 wakiwa na umri kati ya miaka 15-64.
“Tija ya watu husika ni muhimu sana katika kuleta maendeleo ya mkoa husika mathalani kwa taifa la Rwanda kwa sasa linaonekana kuwa na uchumi mzuri likiwa na idadi ya watu wachache na eneo lake dogo, lakini hali ya uchumi wake ni mzuri huku kwa mwaka 2026 Rwanda ina watu milioni 14.3 na ukubwa wa KM za mraba 26.34 tu. ”
Haya ni kulingana na Jonathan Rasiheri Kimaro Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji na tathmini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa mwaka wa 2026.
“Wingi wa idadi ya watu wa mkoa, wilaya au eneo lolote hauwezi kutoa ishara ya uchumi wa eneo bali kikubwa ni ubora wa aina ya watu hao yaani wanajishugulisha vipi katika majukumu ya uzalishaji mali?”
Mkoa wa Mara ni muhimu kiuchumi na kijamii kutokana na rasilimali zake za asili, hususani uwepo wa Ziwa Victoria, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, madini, hali ya hewa, kilimo na ufugaji huku Mkoa huu unapakana Kaskazini na Kenya , Mashariki: Mkoa wa Arusha , Kusini: Mkoa wa Simiyu na Magharibi: Ziwa Victoria nayo Makao makuu yakiwa kando ya Mlima Mukendo Musoma Mjini jirani na mwalo za Ziwa Victoria.
Nayo Historia haijautupa mkoa huu inadokeza kuwa:
“Waruri, Wajita na Wakwaya wanapotamka neno Omusoma wakimaanisha sehemu ya nchi kavu iliyoingia ziwani, yaani RASI na hapo ndipo neno MUSOMA likaibuka, haya ni ya enzi hizo na sasa jina hili ni wilaya mojawapo ya Mkoa wa Mara.”
Mkoa huu umegawanya katika wilaya sita nazo ni:Tarime, Rorya, Serengeti , Bunda, Butiama na Omusoma (Musoma) zikijengwa katika Halmashauri tisa ambazo ni Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Mji wa Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Wilaya na Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Ukitazama idadi ya watu , Halmashauri yenye watu wachache ni Mji wa Tarime ikiwa ni watu 153,673 huku wanaume 73,623 na wanawake ni 80,548 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ndiyo kinara yenye watu wengi ambao ni 465,410 wanaume 226,529 na wanawake ni 238,181. Katika takwimu hizo zote swali la kujiuliza inakuwaje Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ina watu wengi kuliko Halmashauri zote za Mkoa wa Mara?
“Mgodi Mkubwa wa Dhahabu wa Barick North Mara, uwepo wa migodi mingine midogo midogo, uwepo wa ujirani na mpaka na nchi jirani na Kenya na hata uwepo wa misimu miwili ya kilimo ule wa mwezi Agosti hadi Disemba na ule wa mwezi Februari hadi Juni.”
Haya ni kwa mujibu wa Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ndugu Zakaria Sendema kwa mwaka wa 2026.
Kwa hakika hali ya hewa ya mkoa wa mara ikiwa na wastani wa nyuzi joto 20-30 huku mvua za misimu miwili (masika na vuli) mkulima akiwa na nafasi ya kuchagua cha kupanda kwa msimu anaoutaka na kizuri zaidi uwepo wa hali hii ya hewa unafaa kwa kilimo na ufugaji.
Sekta ya Kilimo ambayo inakusanya mazao, mifugo, misitu, mazao ya nyuki na uvuvi inachangia asilimia 48 ya uchumi wa mkoa. Katika mchango huu Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ndiyo inayochangia zaidi katika asilimia hizo ambapo inaingiza asilimia 10 huku asilimia 38 zinachangiwa na Halmashauri zingine nane.
Nako katika pato la taifa kwa mwaka wa 2020 ilichangia Trioni 2.5 na kwa mwaka wa 2024 imechangia trioni 3.5 hapa kukiwa na ngezeko la Trioni moja. Wakati wa upande wa Viwanda , Ujenzi , Madini na Maji kwa mwaka wa 2020 Mara iliingiza trioni 1.1 na kwa mwaka wa 2024 waliingiza trioni 1.5 kukiwa na ongezeko wa trioni 0.4 yaani bilioni 400.
“Kwa upande wa huduma za kijamii kwa mwaka wa 2020 ilingiza trioni 1.8 na kwa mwaka wa 2024 iliingiza trioni 2.5 kukiwa na ongezeko la trioni 0.7 ambayo ni sawa na bilioni 700.”
Haya yote ni kulingana na Issa Rajabu Mbombwe ambaye ni mchumi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika Mkoa wa Mara una rasilimali nyingi zinazoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jukumu lako wewe unayetaka kuwekeza ni kuchagua tu pa kuwekeza iwe katika kilimo, mifugo, uvuvi, utali, madini au sekta yoyote ile uwanja ni wako.
Hayo ni machache kati ya mengi kulingana na Ripoti ya Pato la Mkoa wa Mara mwaka wa 2024, Ripoti ya Makadilio ya Idadi ya Watu kwa Mkoa wa Mara 2023-2050, Ripoti ya Idadi ya Watu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime 2023-2050 na Wataalamu kadhaa wakiwamo wachumi, watakwimu na maafisa mipango Ofisi ya Mkoa wa Mara kama walivyoeleza mbele ya Mwanakwetu kwa mwaka wa 2026.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Ougemenya Mkoa Gwa Mara- Unaufahamu Mkoa wa Mara?”
Nakutakia Siku Njema
makwadeladius @gmail.com
0717649257










.gif)
Post a Comment