Adeladius Makwega-MBAGALA
Msomaji wangu nakualika tena katika Makala ya Katuni Siku ya leo, kumbuka haya ni Makala ya Uchambuzi wa Katuni kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji wa katuni hizo kutoka vyanzo mbalimbali. Kumbuka ndani ya makala haya zinachaguliwa Katuni nne kisha zineleezewa namna zilivyo alafu zinafanyiwa uchambuzi kwa jicho la mtayarishaji wetu.
Kuyaanza makala haya siku ya leo Mwanakwetu anaikamata katuni ya kwanza kabisa ambayo imechorwa na Godfrey Mwapembwa maarufu kama GADO ambapo anaonesha mandhari ya mahakamani ambapo hakimu yu kazini na jamaa mwenye shati lililobandikwa maneno No Reform No Election mtuhumiwa kizimbani.
Mkono wa hakimu unanyanyuliwa na kamba maalumu ambayo inaungana na picha ambayo ipo juu ya mahakama ambayo inamuonesha mama mmoja aliyevaa hijabu maridadi.
Kwa kuitazama katuni hii inaelezea hali ya shauri la Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ambaye anakabiliwa na shauri la uhaini huku akiwa Korokoroni kwa sasa. Kwa mujibu wa katuni hiii Godfrey Mwampembwa anajenga hoja kuwa mahakama katika katuni hii inapokea maelekezo kutoka katika sanamu juu yake huku akiipa picha katika flemu vitendo vya binadamu aliye hai.
Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya pili ambayo imechorwa na Nathan Mpangala, katuni hii inaonesha jamaa mmoja ameinama katika bonde moja hatari, huku akivutwa atumbukie chini shimoni. Katuni hii inapotazamwa kwa jicho la mtayarishaji wetu inaonesha taswira na mandhari ya ajali za barabarani ambapo zinasababisha vifo vya watu wengi sana dunia., takwimu zinadokeza kuwa katika kila baada ya dakika 40 mtu mmoja anafariki kwa ajali, takwimu za ajali zinadokeza zaidi na kuipiga kengele ya hatari kwa kunadi kuwa ajali ni sababu namba tisa inayosababisha vifo vingi duniani.
Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya tatu ambayo imechorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji wa Ujerumani DW Kiswahili, ambapo kunaonekana miradi kadhaa inayofadhiliwa na Ulaya na Marekani ; zahanati na shule huku akina mama wakiwa foleni na katika zahanati hii na wanafunzi wakiwa shuleni wakisoma, kando ya miradi hii kipo chooo alafu kwa kando yupo mama mmoja aliyevalia hijabu nyekundu na baibui nyeusi huku akisema maneno kuwa Ulaya na Marekani hawafanyi vizuri huku sisi tunafanya vizuri.
Mtayarishaji wa makala haya bado anaitazama katuni hii kwa kina huku taswira ya huyu mama inafanana na ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, swali la kujiuliza je ni kweli mataifa ya Afrika yanafanya vizuri zaidi ya Marekani ana ulaya? Huku nyuma ya pazia mataifa ya Afrika yakiendelea kupokea misaada ya miradi kadhaa kutoka Ulaya na Marekani.
Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya nne na ya mwisho ambayo imechorwa na Masoud bini Kipanya. Hapo kunaonekana jamaa wawili wamekaa katika dawati maalumu wakiwa na bakuli kubwa na kando jamaa hawa wakiwa wameshahesabu fedha na fedha yenyewe ni kidogo mno , jamaa hawa wapo njia panda.
Kwa jicho la mtayarishaji wetu tafsiri ya katuni hii zipo nyingi sana kulingana na jicho la anayetazama, Mwanakwetu amechagua tafsiri hii ya Emmanuel Kaswanya;
“Hapo ni kwamba, sisi tunadai uchumi wetu ni mzuri kuliko wenzetu wa Marekani na Ulaya ilhali bakuli liko empty(tupu) na mtoto kakaa pembeni anasubiri kauli ya baba ili apate kushiba! Na baba kakata tamaa maana uelekeo wa kupata chochote katika bakuli ni zero!Na ukumbuke hao tunaosema hawafanyi vizuri ndio hao hao wanaotudai madeni ya kila mtanzania lukuki,!!!!inafikirisha sana nchi hii Mungu atupe uvumilivu.”
Mdau mwingine katika katuni hii akauliza Lo salale Umejumuika na Walioharibu Kwao?
Mwanakwetu siku ya leo alikutana na picha moja nzuri iliyomvutia ambayo inayomuonesha Shekhe Issa Ponda ankiwa na Baba Askofu Mwamakulwa katika mojawapo ya mkutano wakifuatilia jambo kwa umakini mkubwa.
Basi msomaji wangu hadi hapa ndiyo na mimi natia nanga ya Makala ya Katuni siku ya leo, kumbuka Mwanakwetu alikuwa na katuni nne; ile ya GADO mandhari mahakamani, ile ya Nathan Mpangala na ajali za barabarani , hii ya Ulaya na Marekani hawafanyi vizuri kama sisi na katuni ya mwisho ni hii ya Wazee wa Kutembeza bakuli.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Umejumuika na Walioharibu Kwao.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment