MZANI HAUPO SAWA

 


Adeladius Makwega-MBAGALA

Msomaji wangu nakualika tena katika Makala ya Katuni, haya yakiwa makala ya uchambuzi wa katuni moja baada ya nyingine, huku katuni husika ikielezewa maudhui yake namna yalivyo kwa jicho la mtayarishaji wetu. 

Siku ya leo Mwanakwetu yupo kigulu na njia akizunguka katika ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ali Possi kama nilivyotoa ahadi katika makala zilizotangulia nipo kidhahania.

Kuyaanza makala haya huku Mwanakwetu akiwa ameshiba Pilau ya Idd ya Sheikh wa Mkoa wa Mara lililopikwa na akina wa Kikulya na Kijita anaikamata katuni ya kwanza ambayo imechorwa na Masoud Bini Kipanya huyu ni al Ustadh ambayo inaonesha kipanya yu mwanae, mtoto wa Kipanya anamuuliza Baba yake hivi Kirefu cha CHAUMA ni nini?

Mtoto wa Kipanya anangoja jibu . Kwa kando Kipanya anajibu kuwa Kirefu cha CHAUMA ni Chama Cha Ubwabwa na Maharage. 

Lo salale), kumbe CHAUMA ni Chama cha Ubwabwa na Maharage.

Katuni hii inaelezea hali ya siasa ya Tanzania juu ya Chama hiki Cha CHAUMA , huku Watanzania wakiwa na maswali mengi Je CHAUMA kimepata wapi fedha cha kuwezwa kuwa na magari na hadi kukodi Hedikopta? 

Je viongozi wa CHAUMA wameokota TANZANITE mchangani? Kama wameokota mbona Mwanakwetu haokoti?


 

Jambo hili linaibua maswali na linakosa majibu, huku baadhi ya wadau wakiona kuwa chama cha CHAUMA kinapewa nguvu ili kuwaadaa wapiga kura tu na  si chochote si lolote.

Mwanakwetu sasa anabisha hodi katika Ofisi ya Naibu Wakili Mkuu Bi Alice Mtulo huku akingoja majibu ya hodi yake, huku anaikamata katuni ya pili ambayo imechorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani-DW KISWAHILI. 

Katuni hii inaonesha jamaa yupo njia panda huku jamaa huyu kapewa maandishi G 55 yaani wale CHADEMA waliokikimbia chama hiki wangini wakienda huko CHAUMA chama cha Ubwabwa na Maharage kama anavyosema Masoud Kipanya.

Katuni hii inaonesha kuwa jamaa hawa wapo njia panda wakiangalia pahala pa kwenda huku kukiwa na maglovsi ya kupigania kadhaa ambayo yamepewa majina ya vyama kadhaa vya nchini Tanzania ikiwamo CCM, Mwanakwetu anakumbuka maneno ya Babu Duni Haji juu ya CCM A , CCM B na CCM C.

Mchoraji wa katuni hii anaonesha njia ya panda ya jamaa hawa, huku kukisikika maneno kuwa ingekuwa heri kama kungekuwa na mgombea binafsi.

Katuni hii inajieleza vizuri, hakuna haja ya kuiongezea maneno lakini kubwa ni suala la Mgombea Binafsi nalo lina maantiki si kwa ngazi ya Urais tu , bali hata ngazi ya Ubunge , Udiwani na hata ngazi ya Uenyekiti wa Serikali za Mitaa. 

Hili litaondoa mizengwe ya vyama vya siasa katika uchaguzi .Maana chama cha siasa ni dhahania, jambo la msingi ni nia njema ya hao wanasiasa waliyo pamoja.

Mwanakwetu bado anabisha hodi ofisi ya Naibu Wakili ya Wakili Mkuu na hapa hapa anaikamata katuni ya tatu ambayo nayo imechorwa na Said wa Michael wa DW Kiswahili hapa kunaonekana Mwanasiasa akirudi jimboni, nadhani huyu jamaa alikuwa Mbunge, sasa anarejea jimboni akiwa na rundo la fedha na sufulia iliyojaa minofu tele ya nyama . Mwanasiasa huyu anasema kuwa ukisikia mpango mkakati ndiyo huu, maana yake rushwa ndiyo mpango mkakati wa uchaguzi nchini Tanzania.


 

Kwa mbele ya kiongozi huyu kuna bomba la maji halitoi maji huku kuna foleni ya ndoo kadhaa. Wananchi wake mafukara mno huku wakisema msimu wa ahadi umefika.

Kwa hakika hii ndiyo ya hali ya siasa ya Tanzania ilivyo kwa miaka mingi kila uchaguzi ukifika, kwa hakika rushwa kwa wanasiasa ni jambo ambalo linafanyika bila aibu huku Tanzania ikiwa na vyombo kadhaa vinavyopambana na rushwa. Ebu tuone rushwa mwaka huu inaweza kupata mwarubaini wake hasa ndani ya CCM kwenye kura za maoni?

Mwanakwetu anajiuliza ukifika Wakati wa Uchaguzi Tanzania TAKUKURU Inakuwa Likizo?


 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya nne na ya mwisho siku ya leo ambapo imechorwa na GADO ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Kenya, huku akiifanya vizuri kazi ya kuchora katuni hizo. 

Katuni hii inaonesha kunafanyika dibeti ya uchaguzi nchini Tanzania na kuna marufaa mbili, marufaa ya kwanza kasimama mama aliyevaa hijabu na marufaa yake imepewa jina SAMIA na kando kuna marufaa ya pili imepewa maneno LISSU lakini kando ya marufaa hii hakuna mtu anayeoneka bali kwa mbali kunaonekana kuna jamaa anapigwa na mawe, anapigwa na kitako cha bunduki akiwa amelala chini akipokea kipigo.Lo salale jamni mtamuua bure, huyu ni mwanasiasa tu siyo mharifu.

Mwanakwetu anapoitzama katuni hii inaonesha hali ya uwanja wa siasa ulivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 hasa kwa nafasi ya Urais , swali ni je mzani upo sawa? Kwa hakika msomaji wangu jibu unalo na hapa Mzani Haupo Sawa.

Katuni hii ya GADO na anavyofanya kazi yake ya Uchoraji wa Katuni inaonesha udugu baina ya Kenya na Tanzania na inamkumbusha Mwanakwetu Julai 20, 2020 ambapo Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa alifariki dunia, Ben Mkapa alikuwa rafiki wa Mwanakwetu na alikuwa anampenda sana Mwanakwetu akimuita Ahaa Mwanakwetu! ,Ahaa Mkurugenzi Kazimbaya! huku mimi nilikuwa awali nilikuwa nikimuogopa sana lakini baadaye nikamzoea sana. 

Siku ya leo nakukumbusha jambo moja zuri ambalo Serikali ya Jamhuri ya Kenya chini ya Rais wa Kenya wa Wakati huo Uhuru Kenyatta ililifanya baada ya Kifo cha Ben Mkapa iliwatangazia Wakenya siku tatu za maombelezo kwa msiba wa mzee wetu Ben Mkapa.

Hilo ni tukio nadra sana kufanyika kwa taifa lingine, kwa kiongozi ambaye hajawahi kuongoza taifa linalofanya maombolezo kwa siku moja, mbili hadi tatu . Anaweza kufariki rais wa taifa jirani, watu wakatuma Balozi kusaini Kitambu cha Maombolezi tu Ubalozini kisha wanaendelea na mambo yao. Kikubwa ni mchango wa Ben Mkapa aliposhiriki kutatua mgogoro wa kisiasa wa Kenya katika mojawapo ya uchaguzi ulioleta balaa nchini Kenya.

Kumbuka Makala ya Katuni siku ya leo yalikuwa na Katuni nne , ile ya Chama cha Ubwabwa na Maharage , ile ya G 55 na ya tatu ni ya Rushwa na Likizo ya TAKUKURU na katuni ya nne ni hii ya GADO ambayo imemkumbusha Mwanakwetu siku tatu ya maombolezo baada ya Kifo cha Ben Mkapa huko nchini Kenya.


 

Je makala haya niyaitaje? Chama cha Ubwabwa na Maharage? Likizo ya TAKUKURU? Mzani Haupo Sawa? Mwanakwetu anachagua Mzani Haupo Sawa.

Makala haya Mwanakwetu ameyatayarisha spesheli akiwa kidhahania kando ya Ofisi ya Bi Alice Mtulo Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Mtumba Mji wa Serikali. 

Naweka chini kalamu yangu chini huku nikikuomba msomaji wangu uyatafakari yote uliyoyasoma katika makala haya.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka Mzani Haupo Sawa

Nakutakia siku njama.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 








0/Post a Comment/Comments