ZIZI LENYE MASHAKA

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Nakualika tena katika Makala ya Katuni siku ya leo, Kumbuka haya ni Makala ya Uchambuzi wa Katuni kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji mbalimbali wa vibonzo hivi katika vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania na ulimwenguni kote.

Kuyaanza makala haya Mwanakwetu anaikamata katuni ya kwanza ambayo imechorwa na King Kinya hapa kunaonekana jamaa anakomelea na kugongelea kibao kimoja kilichopewa jina KIZIMKAZI huku kwa kando kunaonekana kibao kilichopewa jina CHATO na kimevunjika kabisa na kimelala chini chali kifo cha mende.

Mtayarishaji wa Makala haya anapoitazama kazi hii ikamjia akilini mwake LUPASO kisha MSOGA na Baadaye KISEVULE na pia BUTIAMA. Majina hayo yote sita yakitaja nyumbani kwa marais waliowahi kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mtayarishaji wa Makala haya anapoitazama katuni hii ainakuja na hoja ya maeneo ambayo viongozi wakubwa wa taifa hili wanatokea, yamekuwa yakitazamwa na baadhi ya watu kuwa maeneo haya kana kwamba yanapendelewa baadhi ya miradi ya maendeleo na hili likiwa jambo baya ambalo halifai, wanaolalamika wakiomba kuleta usawa wa maeneo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hilo likiwa jukumu la kila kiongozi.

 


 

 

 

Mtayarishaji wa Makala haya anaigonga kengele na kukumbusha kwa kila kiongozi, hali hii mtayarishaji wa makala haya anaona haifai na lazima hilo lipingwe ili kuondoa fikra hizi kwa Watanzania.

Sasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya pili ambayo imechorwa na Alwatan Masoud Kipanya, katuni hii inamuonesha jamaa yupo katika kijibanda kama cha Uhamiaji, eneo kama la Uwanja wa Ndege, huku akimuuliza mgeni aliyefika uwanja wa ndege maneno haya unakuja Tanzania ku wuk yaani unakuja Tanzania kufanya kazi au unakuja Tanzania kuwuk yaani kutembea? Huyu jamaa anayeulizwa mwenye sura kama ya Kizungu anajibu kuwa anakuja Tanzania kufanya kazi na kutembea pia.

Kwa hakika mchoraji wa Katuni hii anaibua dhana ya mtumishi huyu wa uhamiaji anashindwa kutofautisha maneno haya mawili ya Kimombo Work ya Kazi Walk ya kutembea lakini pia katuni hii inaibua dhana ya pili juu ya wageni wanaoingia Tanzania japokuwa wanaweza kuja kufanya kazi lakiani pia wanakuja kutalii hivyo tukae nao vizuri.

Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu ambayo imechorwa tena na Alwatani Masoud Kipanya ambapo kunaoneka kundi la wanyama kama Kondoo vile , wapo zizini na kama hawana mchungani, huku muda wa machungoni umefika, wanajianda wenyewe kwenda wa kwanza mbele, hakuna mchungaji wala nani , Ebooo hii ni hatari sana.

Mtayarishaji wa makala haya anaibua dhana ya usalama wa kondoo hawa upo mashakani, kondoo hawana mchungaji akiibuka fisi, akiibuka simba , akiibuka mnyama mkali anajitwalia mmoja au wawili na kuondoka zake ndiyo kusema zizi hili si salama.Taswira kubwa lazima kundi la kondoo liwe na kiongozi makini anayewapenda mifugo yake na lazima awepo mchungaji mwema ili kulipa uhakika wa usalama kundi hilo la kondoo.


 

Katuni hii inatoa nafasi ya Mwanakwetu kuikamata katuni ya nne nay a mwisho iliyochorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani ambayo inazungumzia hali ya Tanzania mara baada ya wahuni kuingia katika akaunti za Twiter yaani X za taasisi za umma Tanzania na kuandika mambo yasiyofaa dhidi ya viongozi wetu. Hali ilifanya mamlaka ya mawasiliano ya Tanzania kuufungia mtandao huo.

Swali ni je ilikuwa halali kwa mamlaka ya mawasiliano Tanzania kuufungia mtandao huu wa Twitter baada ya tukio hilo?

Mwanakwetu anajibu kuwa hilo halikuwa halali kikubwa TCRA inawajibu wa kujipiga picha kutitathini na kuangalia je uwezo wa maafisa wetu katika taasisi hizo juu ya ulinzi wa taarifa za kimtandoa ukoje? Kisha wangetoa mapendekezo kwa taasisi hizo pengine hata TCRA maafisa wake wangetoa ujuzi wa kutosha ili kuepuka hali hii isitokee tena.

Kitendo cha kufungia Twitter hilo ni kosa kubwa hasa kibiashara, maana sasa mitando hii inatumika kwa shughuli mbalimbali.


 

Huku mitandao hii ya kijamii kwa sasa ni ajira kubwa inayowaingizia vipato wanajamii wote na kilichotokea inawezekana kikawa uzembe maafisa wa taasisi hizo kwa kutokuwa makini kulinda taarifa zao.

Mwanakwetu upo ?

Basi hadi hapo msomaji wangu ndiyo natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo. Kumbuka nilikuwa na katuni nne ile Kizimkazi na Chato , ya pili ni ile ya Kuwuk wuk na katuni ya tatu ni hii ya Zizi Lenye Mashaka na katuni ya nne ni hii ya TCRA kuufungia mtandao wa Kijamii wa Twiter nchini Tanzania.

Hapo ndiyo kituo cha makala haya siku ya leo.

Kumbuka

“Zizi Lenye Mashaka.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

 

0/Post a Comment/Comments