WASIOJULIKANA WAPO MASHAKANI


Adeladius Makwega-MBAGALA

Ni majira ya asubuhi ya Mei 18, 2025 Mwanakwetu anawasiliana na jamaa yake aliyekuwepo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Mkoani Kilimanjaro na kisha kumueleza kama hautopata huduma haraka nakumuomba awasiliana na Gabrieli Chisseo yeye ni Afisa Habari wa muda mrefu wa taasisi hii ya Tiba inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT). Jamaa huyu wa Mwanakwetu akasema anamfahamu ndugu Gabrieli Chisseo, akiungama kwa Mwanakwetu kuwa kama hatopata huduma kwa haraka atamuona ili amsaidie.

Mwanakwetu akampa lakini hii huyu jamaa yake;

“KCMC ni miongoni mwa taasisi zinazomilikiwa na Kanisa la Martin Luther, hawawezi kuwa watu wababaishaji, watu wa danadana, utapata huduma mapema.”

Je ni kweli Ndugu wa Martin Luther wapo vizuri?

Mwanakwetu aliendelea na majukumu yake hapo kwake, kisha majira ya mchana akakumbuka kumpigia simu yule jamaa yake aliyekuwa KCMC, simu ilipopigwa kwanza ilikuwa inatumika lakini baadaye akapokea akisema,

“Tupo Mwanga, kuna kijana wa kaka anasoma, tunamsalimia pale KCMC tulipata huduma muda ule ule na kuanza safari ya kurudi Lushoto Mkoani Tanga, unajua nilisahau kukujulisha hilo.”

Mwanakwetu akasema kimoyomoyo, kumbe ni kweli ndugu wa Martin Luther wako vizuri. Mwanakwetu akaendelea na shughuli zake hapo kwake na ilipofika majira ya gizagiza njaa ikamuuma, hapo akakata shauri aende kula pahala fulani, akafika mkahawani, huku wateja kadhaa wakipata huduma hii ya chakula. Eneo hili lilikuwa na wahudumu wa aina mbili wavulana na wasichana huku mpokea fedha dada mmoja peke yake.

“Dada mmoja mrefu, maji ya kunde, mwembamba , akiwa na miguu ya bia, dada huyu kaumbika vizuri sana na anapendeza sana pale unapomsanifu (kumtazama) tangu unyayo hadi unywele.”

Mwanakwetu hapa mkononi ana noti ya shilingi 10,000/= akafika na kumpa kijana mmoja ambaye ni muhudumu lakini huyu kijana inavyoonekana hapaswi kupokea pesa.Kijana aliyepokea pesa akasema maneno haya,

“Eliza pokea pesa yako muhudumie huyu mteja anataka hiki na kile.”

Elizabeth alimtazama huyu kijana kwa jicho pembe, kana kwamba hakuridhishwa, pengine alisema kimoyomoyo labda akisema inakuwaje huyu mteja anampa pesa huyu kijana na hanipi mimi? Mwanakwetu akaenda kukaa katika kiti lakini muungwana Mwanakwetu analo la moyoni juu ya huyu dada Elizabeth Mkahawani huku akiwa na sababu kubwa ya kukataa kuwa jirani na Eliza.

Katika eneo alilokaa Mwanakwetu mkono wake wa kulia kulikuwa na vijana wawili mmoja kavaa fulana nyeusi na mwingine shati lake lilikuwa la rangi ambayo haikukoza sana kama rangi ya tumbaku kavu wanakula, kijana huyu akawa anasema

“Tangu jana Interneti ya simu inasumbua shida ni nini? Yaani nimepekua video ya Mchungaji wa Huduma ya Kristo aliyetekwa nisikie anasema nini hadi sasa ndiyo naweza kuicheza.”

Msomaji wnagu Mwanakwetu yu mkahawani hapa, anaona watu wengine wanapewa huduma lakini yeye hapewi huduma yoyote japokuwa amelipa pesa yake kwa huduma hiyo. Jamaa hawa kando ya Mwanakwetu wanasikiliza video hiyo, hapo hapo Mwanakwetu akaagiza soda na Mungu bahati kijana wa soda akafika na kumpa kinywaji chake huku akinywa kidogo kidogo na jamaa hawa kando wakawa wanaongea.

“Haya mambo ya utekaji yanasumbua sana, unajua sasa ninaona hata utaratibu wa utoaji wa FOMU NAMBA TATU, Bunge lingeamua fomu hiyo mtoaji angekuwa MAHAKAMA YA TANZANIA, Jeshi la Polisi Tanzania lingepokonywa kazi hiyo na hata hizi huduma za matibabu iwe katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali ambazo zipo katika vyombo vya ulinzi ,Bunge lingeagiza zikabidhiwe kwa Halmashuari na Wizara ya Afya , huku watumishi wa Serikali wawe watoa huduma na hata kama wapo watumishi wa vyombo na wao wafanye kazi lakini ziwe chini ya utawala wa kiraia na siyo uongozi wa vyombo vya ulinzi tena. Bajeti za huduma hizo zipitie Halmshauri zilipo  hizo zahanati na vituo cha afaya na zile Hospitali kubwa ziwe chini ya Wizara ya Afya.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu mkahawani anakunywa soda yake na huyu dada hajamletea Mwanakwetu chakula chake hadi sasa sijuhi kasahau nini. Jamaa hawa wanaendelea kuongea,

“Hili zoezi la utekaji kwa ninavyoliona, hata watekaji inaonekna wanaumia , kupata hata vilema na hata pengine kufa katika zoezi hili, kwa sababu hakuna bindamu ambaye ametekwa anaweza kukubali kufa kizembe hata kama amefungwa pingu, lazima binadamu atahangaika kuipambania nafsi yake, maana yake waliokando (yaani watekaji ) hawako salama.”

Jamaa kando ya huyu ndugu akasema maneno haya,

“Unajua hawa watekaji wanafanya utekaji sawa, ukiona mazingira ya tukio unaona damu nyingi, maana yake hata damu hizo zinawarukia na pengine hawa watekaji wanaambukizwa  hadi magonjwa katika zoezi hili. Ebu fikiria madaktari tu wakiwa kazini na wamejikinga lakini wanaambukizwa magonjwa sembuse wewe mtekaji? Haya mambo yana madhara makubwa.”

Mwanakwetu akashituka mno maneno haya makini yaliyokuwa yanazungumzwa na ndugu hawa, kwanza akahisi hawa vijana ni kama madaktari lakini hakuweza kupata uhakika wa jambo hili. 


 

Msomaji hadi wangu hadi hapo dada Eliza hajaleta chakula kwa Mwanakwetu hapa mkahawani. Jamaa wale wanaongea sasa Mwanakwetu hapa hata njaa imekata maana maelezo ya hawa vijana yalikuwa matamu sana, akiyasikiliza kana kwamba hayasikilizi vile.

“Unajua hawa watekaji kama wamekwenda kumteka jamaa, kisha zoezi lao likagonga mwamba wanabaki salama? Unajua kwa hali ilivyo sasa hata hawa watu wanaouwawa wanaosema majambazi pengine ni sehemu ya watekaji na pengine mambo yaligonga mwamba.”

Jamaa wanaongea kwa uhuru kabisa na kisha wakasimama na kweneda kunawa na kuondoka zao. Walipoondoka hawa vijana Mwanakwetu akamsitua kijana mmoja muhudumu amwambie Dada Eliza kuwa hajamletea chakula karibu dakika 15 sasa, Eliza alishituka akaomba sana msamaha na kisha kumletea chakula Mwanakwetu na yeye kula.


 

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba nikupe siri ya kweli ya Eliza Muuzaji wa Chakula hapa Mkahawani. Huyu Eliza alivyoumbika anafanana kila kitu na yule jamaa wa Mwanakwetu aliyekuwa KCMC ambaye aliyezungumza na Mwanakwetu juu huduma za pale KCMC na baadaye kumwambia wamepata huduma na wako Mwanga na huku wale Jamaa wa Martin Luther walivyowapa huduma vizuri.

Haya msomaji wangu ni ya sirini kabisa hata Dada Eliza Muuzaji Mkahawa hajui, sasa nikumegee zaidi;

“Unapomuona mtu wa jinsia nyingine na wewe, unampenda na pengine akifanana na mtu unayempenda sana, jitahidi kutomuweka karibu, awe mbali sana na wewe ili shetani asikuingie na wewe ukaivunja amri ya Mungu.”

Msomaji wangu fahamu kuwa nayeye Mwanakwetu ni binadamu, alikuwa chakula hicho vizuri na hata alipomaliza kula, kupewa chenji ilitumia muda mrefu sana kama dakika tano hivi, Eliza akisubiri nimuombe cheji yangu huku Mwanakwetu akitumia mtindo wa kia ofu akamuagiza kijana yule wa awali.

“Mwambie Eliza Naomba cheji yangu.”

Eliza alitoa cheji huku akiomba msamaha mara mbili mbili kwa kuchelewa, Mwanakwetu aliaga na kuondoka zake na baadaye kuamua kuyaandika makala haya.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika hapa mambo ni mawili tu kwanza umeona Watanzania wnavyolijadili suala hili la watu wasiojulikana? Kwa kifupi Watanzania wanaipenda nchi yao, jukumu la viongozi kujiuliza wanaamua nini juu ya hali na mustakabali wa taifa hili kwa sasa?

“Fomu namba tatu itolewe na Mahakama ya Tanzania na vyombo vya Ulinzi visimiliki taasisi yoyote ya tiba.”

Huu ni ushauri wa wadau hawa, Wewe kama kiongozi lazima ujiulize jamii ina hisi nini katika hali kama hii? Jamani tuoneane huruma tangu wanaoteka watu na hawa watekaji wenyewe hawako salama kama kuambukizwa magonjwa, mengi mathalani Homa ya Ini, wewe unaomvamia tu kila mtu kuwa makini ! Magonjwa ni mengu .Hata Watekaji Wako Mashakani.

Mwisho, mwisho ,mwisho ni juu ya Mwanakwetu na Dada Eliza hapa mkahawani hapa niseme haya,

“Kumbuka sana mtu anayefanana na unayempenda, usimuweke jirani na wewe.”

 

Mwanakwetu upo ?

Je makala haya niyaitaje?

Fomu Namba Tatu Itolewe na Mahakama, Vyombo Vyetu vya Ulinzi Visitoe huduma ya Afya, au Watekaji Wako Mashakani?

Mwanakwetu anachagua Wasiojulikana Wapo Mashakani

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB Makala haya yameandikwa MwAnAkWeTu kwa heshima zote kwa Mchungaji Steven Jacob wa Kanisa la Huduma ya Kristo aliyetekwa  hivi karibuni, tunamuombea apone  haraka.



 
















 

 




0/Post a Comment/Comments