USHIRIKA NI BIASHARA-JUKWAA LA USHIRIKA MKOA WA MARA

Adeladius Makwega-Musoma Mara

Jukwaa la Ushirika Mkoa wa MARA ni tukio muhimu linalofanyika kila mwaka kwa lengo la kuimarisha na kukuza vyama vya ushirika katika mkoa huo. Tukio hili linawahusisha viongozi, watendaji, na wanachama wa vyama vya ushirika wa aina mbalimbali, vyama vya akiba na mikopo, pamoja na wadau wengine.

Katika Jukwaa hili, viongozi wa ngazi mbalimbali hutoa wito na maelekezo muhimu kwa wanachama wa ushirika.

Mathalani, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ambaye ni mdau nambali moja na Kiranja wa Ushirika, katika kila vikao vyake ndani na nje kwa jamii ya watu wa Mara  amekuwa akipiga mbiu yake ya mgambo kila mara kuwaomba wana wa ushirika kuhakikisha ushirika unakua na kuimarika maradufu.

“Mkoa wa Mara una utajiri mkubwa na wa njenje, fursa zipo kila kona, fursa tele kama umaskini ni wa kujitakia.”

Haya yamekuwa yakisema kila Mara na Mhe.Kanali Evans Mtambi akionesha kuwa mstari wa mbele katika kulenga shabaha ya kuzifikia fursa kadhaa za uchumi kwa wana wa Mara.


 

Kwa hakika Kanali Mtambi amekuwa kinara wa kuyaunganisha makundi kadhaa ya wana Mara tangu Vijana, Kinamama na bila kuwasahau Akinababa wenzake huku akisisitiza umuhimu wa makundi yenye mahitaji maalumu kutiliwa maanani zaidi.

Jukwaa la Ushirika Mkoa Mara kwa mwaka wa 2025 linafanyika kwa siku mbili yaani Mei 8 na 9, 2025 huku Mwanakwetu akiwa na matumaini makubwa ya fursa kemkem kuibuliwa na wanajukwa kujenga mtandao mkubwa  zaidi.

Kwa upande mwingine, Katika ufunguzi wa Jukwaa hili lenye kauli mbiu USHIRIKA NI BIASHARA, Mwanakwetu alizungumza kidogo na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele ambapo alionesha matumaini makubwa kwa Jukwaa hili huku akizitazama fursa tele katika Wilaya yake anayoiongoza ambayo ni wilaya yenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu.


 

Maeneo mbalimbali ya ushirika yanashiriki katika Jukwaa hili, ikiwemo vyama vya akiba na mikopo ambapo hushiriki katika mijadala na semina mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma na ufanisi wa vyama vya ushirika

Kwa ujumla, Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara linaendelea kuwa jukwaa muhimu la mafunzo, mijadala, na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika katika mkoa huu likiwa mwanga mkubwa kwa mkoa huu wenye utajiri wa Madini, Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Biashara na mataifa ya Kenya na Uganda.

Dawati la Mwanakwetu ndani ya jukwaa hili lina matumaini makubwa zaidi na wana Mara kuendelea kushamiri katika fursa hizo.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Ushirika Ni Biashara–Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Mara.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

0/Post a Comment/Comments