Adeladius Makwega-MBAGALA
Mwanakwetu yupo nyumbani kwake na haya yalikuwa majira ya jioni hivi, mara akapigiwa simu na namba ambayo haipo katika kitabu cha simu yake.
“Mwanangu hujambo? Unaendeleaje?”
Mwanakwetu akajibu anaendelea vizuri, kisha akauliza nani mwezangu?Jamaa akajibu
“Mimi ni Baba yako Mdogo, Abeli Herman Makwega? Hujambo tena mwanangu!”
Mwanakwetu akajibu hajambo na kumpa Shikamoo ! Baba yake mdogo. Mzee huyu akajibu salaam hiyo na kisha kuyasema maneno.
“Leo ni Jumapili, nipo kazini, hata kusali Kanisani sikwenda nipo zamu, lakini Mwanangu nimekukumbuka tu, nikasema ngoja nikupigie niongee na wewe. Upo Salama Mwanangu?”
Mwanakwetu akajibu yu salama, mzee huyu akasema,
“Mwanangu kaeni na watu vizuri, hasa watu wa kawaida, watu wanyonge, maana watu wengi duniani wanaheshimu watu wenye nafasi tu, heshimuni kila mtu, bila kujali nafasi yake, uwezo wake au mchango wake kwako.
Unajua nyinyi mmebeba jina letu, likitokea baya watasema Mkina+Makwega kafanya hili na lile. Salaam za ubaya zitavuma hadi kwetu Mrundu Ikangao Ulanga Morogoro zitafika, ni heri uvume kwa wema kuliko kuvuma kwa ubaya maana akina Makwega bado wanazaliwa fikiria tangu akina Peter Makwega Kazimbaya hadi leo ni miaka mingapi?”
Msomaji wangu mzee huyu akaongea mengi, baadaye akaaga na kuendelea na kazi yake ubawabu siku hiyo ya Jumapili.
Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu ninakuomba nimueleze kidogo huyu mzee Abeli Herman Makwega.
“Abeli Herman Makwega anazaliwa Ikangao Mrundi Ulanga mwaka 1965 kwa baba yake Herman Peter Kazimbaya Makwega(Ikangao) na Mama yake anaitwa Katarina Mfaume(Chilombola).
Nikurudishe nyuma kidogo Herman Peter Kazimbaya Makwega anazaliwa ni Peter Kazimbaya Makwega(Ikangao) na Magdalena Nyambuka (Ruaha) ambao walizaa watoto wa kiume sita yaani Herman Makwega, Fidelis Makwega, Otimali Makwega, Alex Makwega, Norbet Makwega na binti mmoja wa kike aitwaye Erika Makwega. Nayeye Mwanakwetu anazaliwa na Mtoto wa kiume wa Fidelis Makwega anayeitwa Francis Fidelis Makwega.”
Herman Makwega Baba Wa Abeli Makwega kumbuka alifunga ndoa na Katarina Mfaume yule bibi wa Chilombola –Ulanga na kuzaa naye watoto sita, nao ni Carolina Makwega, Agwinela Makwega, Akwilina Makwega, Abeli Makwega, Losita Makwega na Domina Makwega. Kwa hiyo Abeli Makwega ni mwanaume pekee yake aliyezaliwa kutoka kwa Babu Mkubwa wa akina Makwega(Herman Makwega).
Japokuwa Abeli Makwega amezaliwa Mwaka 1965 akina Makwega wote tunamuheshimu mno Abeli Makwega kwa kuwa japokuwa Baba zetu wamezaliwa kabla ya Abeli mathalani Francis Makwega mtoto wa Fidelis Makwega alizaliwa mwaka 1950 lakini Abeli Makwega anaheshimiwa mno kwa kuwa anazaliwa na Babu Mkubwa yaani Herman Makwega.
Nakuomba Msomaji wangu sasa nikupeleke kwa Fidelis Makwega yaani Mtoto wa pili wa Peter Kazimbaya Makwega na Magdalena Nyambuka.
“Huyu Fidelis Makwega aliyezaliwa mwaka 1927 alimuoa Hedwiki Omari Binti Mkomangi Mkongeni aliyezaliwa mwaka 1938 katika ndoa yao walizaa watoto kumi ; Francis Makwega(1950)-Baba wa Mwanakwetu, Honesta Makwega, Otilia Makwega, Salome Makwega, Marietha Makwega, Imelda Makwega, Faustina Makwega, Bernadetha Makwega, Corinelia Makwega na Demetria Makwega.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu nyumbani kwake na haya ni majira ya jioni ya Jumapili ya Mei 4, 2025 ambapo awali aliongea na Baba Yake Mdogo anayeheshimika sana Abeli Makwega, kisha Mwanakwetu kuendelea kupitia mitandao ya kijamii ya Tanzania, hapa katika pita pita alikutana na taarifa juu ya kutekwa kwa Mdude Nyagali ambaye ni Mwanasiasa kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA ambaye makazi yake huwa ni Vwawa Songwe na hata Mkoani Mbeya.
Taarifa hiyo ilimkumbusha Mwanakwetu kuwa Mdude Nyagali kwa mwaka 2018 na 2019 pale Vwawa Mbozi alikuwa kijana anayefahamika sana na wakusanya ushuru wa halmashuari ya Mbozi kuwa kama Fundi Redio tu, huku akifanya harakati zake za CHADEMA katika misimamo isiyoyumba.
Mwanakwetu katika pita pita mitandaoni alibaini kuwa wananchi wa mkoa wa Mbeya mara baada ya tukio hili wamekuwa na harakati juu maswali alipo kijana huyu, wakipita wakizunguka mapolini, polisi na wakipanga kufunga safari kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mhe.Juma Zuberi Homera.
Mwanakwetu akiwa kwake alikumbuka kuwa ndugu Juma Zuberi Homera ni Mkuu wa Mkoa Tangu katikati ya mwaka 2019 baada ya kutenguliwa ndugu Amos Makalla akiwa Katavi ambaye sasa ni Katibu Muenezi CCM Taifa. Mwanakwetu alikumbuka pia hata siku Rais John Pombe Magufuli alipomuapisha Jumaa Zuberi Homera kuwa Mkuu wa Mkoa kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya kwa mara ya kwanza Mwanakwetu alikuwepo Ikulu ya Magogoni alishuhudia uapisho huo ulifanyika Mei 16, 2019.
Baadaye Mwanakwetu alikumbuka kuwa pia Agosti 2024 mkoa wa Mbeya ulikumbwa na tukio la kupotea kijana Shadrak Chaula ambaye alitiwa hatiani kwa kuchana picha ya Rais na baadaye mahakama kumuhukumu kifungo au kulipa faini ya shilingi milioni tano, Wasamalia wema walimchangia fedha kijana huyu bahati mbaya kijana huyu alipotoka alitekwa na kupotea hadi kesho haijulikani kama yu hai au la.
Tafakari kubwa ilimjia ndugu yetu Mwanakwetu, Mwanakwetu akiwa kwake alikumbuka majukumu haya ya Mkuu wa Mkoa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
“Ni Kuongoza Kamati ya Mkoa ya maombi ya leseni za magari, Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa inayoshughulikia uteuzi wa vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Pia, ana majukumu ya Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa inayochambua maombi ya watu wanaotaka kuuza dawa zenye sumu,
Na pia Kuongoza Kamati ya kusikiliza rufani za leseni za biashara Mkoani na Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya leseni za vileo. Aidha, anatakiwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mkoa ya utoaji wa leseni za magari na uchukuzi, Na hata Kuteua wakaguzi wa Magereza pamoja na Kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoani mwake.
Mkuu wa Mkoa ni mtendaji wa Serikali anayeongoza Mkoa, anapatikana kwa kuteuliwa na Rais. Pia, anaweza kuteguliwa muda wowote na Rais au akahamishwa Mkoa Mwingine.”
Baadaye Mwanakwetu aliyatafakari yote haya tangu ile simu ya Baba yake mdogo na baadaye matukio ya mkoa wa Mbeya lile la kupotea Shadrak Chaula kisha hili la kupotea Mdude Nyagachi, baadaye Mwanakwetu akakaa akaamua kuyaweka katika maandishi yote hayo na kuwa makala haya.
Mwanakwetu
anasema nini siku ya leo?
Jambo la kwanza kabisa kwako wewe msomaji wangu ukitazama historia ya huu ukoo wa Peter Makwega na mkewe Magdalena Nyambuka walizaa watoto sita; wakiume watano na wa kike mmoja , huku mtoto woa kwanza Herman Makwega na mkewe Katarina Mfaume walizaa watoto saba wa kike sita na wakiume mmoja ABELI aliyempigia simu Mwanakwetu Mei 4, 2024.
Mtoto wa pili wa Peter Makwega yaani Fidelis Makwega na mkewe Hedwiki Omari Binti Mkomangi walizaa watoto kumi; wa kike tisa na wakiume mmoja yaani FRANCIS Makwega-Baba wa Mwanakwetu, nayeye Francis Makwega ana vijana wa kiume watano Adeladius(MwAnAkWeTu) Makwega, Modestus Makwega, Michael Makwega, Samweli Makwega, Juma Makwega na binti mmoja Isabela Makwega.
Jambo la kustajabisha hata uzao wa Mwanakwetu watoto wake wa kuzaa wamekuwa hivyo hivyo mtindo huo huo. Maana yake (tafsiri yake) viko vitu ndani ya miili yetu sisi kama binadamu ambayo tunarithi kutokana na vizazi na vizazi vyetu. Kwa hiyo msomaji wangu vipo vitu tumevibeba kwa nje mathalani majina ya koo lakini vipo vitu ndani ya damu zetu tumevibeba kutoka koo zetu na kama Mungu alivyotuumba, angalia tu huu ukoo wa akina Makwega unavyozaliana tangu mwaka 1880 hadi leo hii 2025 wakivaa watoto wa kike wanazaa watoto wa kike kike wengi na wakizaa watoto wa kiume wanazaa watoto wa kiume wengi. Natambua msomaji wangu hata wewe ukoo wako zipo tabia za aina fulani ebu fuatilia tu utabaini kitu tu.
Jambo la pili msomaji wangu Baba yangu mdogo Abeli Makwega alinikumbusha kukaa na watu vizuri .
“Mwanangu umebeba jina letu, kuwa makini sana katika hilo maana ubaya unavuma kuliko wema, kaa na watu vizuri...”
Katika hili Mwanakwetu anamuomba mhe. Zuberi Omari Homera Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwa
“Tukio la Kupotea Shadrak Chaula hadi leo hii hajulikani halipo halitoi picha nzuri kwake yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya, isitoshe hata hili la pili la Mdude Nyagali na lenyewe linazidi kuchafua jina zuri la akina HOMERA.
Jamii ina mashaka kama Shadrak Chaula alipotea na hajapatikana hadi leo vipi kwa Mdude Nyagachi? Kwa hakika Mwanakwetu anaamini kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya anawajibu wa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakuwa imara bila kujalia itikadi, matamko na misimamo ya wahusika katika jambo lolote lile na kufanya hivyo ni kulinda heshima si ya CCM tu, si ya aliyemteua tu, bali heshima ya UKOO WAKE MAANA AMEBEBA JINALA UKOO WAO kama alivyosema baba yangu mdogo kwamba nyinyi Mmebeba Jina Letu.
KUENDELEA WATU KUPOTEA MKOANI MBEYA MAANA YAKE KUNA KILA DALILI Mteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya afikirie vinginevyo na nafasi hiyo apewe mtu mwingine ambaye atahakikisha watu wa Mbeya wanakuwa salama nduguze JOHN MWAKANGALE na kufanya hivyo ni kutekeleza ilani ya CCM inayonadi kuhakikisha Tanzania inakuwa salama chini ya Chama cha Mapinduzi .
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya afikirie tu Mdude Nyagali na Shadraki Chaula ni ndugu zake wa damu yaani akina HOMERA hawajulikani walipo kibinadamu hali hiyo inakuwaje?”
Kwa hakika ukiutazama Mkoa wa Mbeya na Songwe unao Watanzania kadhaa walioshika nafasi kubwa kubwa serikalini, katika CCM tangu UVCCM mathalani akina Mark Mwandosya na wapo hata waliowahi kushika nafasi Katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na wengine wengi hawa tunawaheshimu, vyovyote iwavyo na hata mtu angeuke vipi watu wa Songwe na Mbeya ni ndugu na hawa viongozi kama kuna tabia tunatafautiana sisi sote ni ndugu na huo ndiyo ubinadamu, kama kuna mtu kakosa kabisa sisi kama Watanzania na viongozi katika maeneo haya tuzungumze na ndugu zao, wao watazungumza kinyumbani kwa lugha ambayo wanaelewana.
Sasa watu wanapopotea kisha haijulikani walipo tafsiri yake kuna pahala mambo yamekwenda kombo.
Kuyaacha haya mambo yabaki kama yalivyo halina tija wala maana , tafsiri yake ipo siku jambo hili linaweza kuligharimu taifa na jata huyu mtu ambaye ni kliongozi kwa uzao wake kuwa baba wa fulani ili lilitokea hakutimiza wajibu. Kwa nini hakutimiza wajibu?
Kama Mwanakwetu anavyochakata katika makala yake juu ya ukoo wake unavyozaliana na hata hili la usalama na watu kupotea linaweza kuchakatwa katika namna nyingine na likaleta shida. Mkuu wa Mkoa Mbeya jitahidi ndugu yetu.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Umebeba Jina Letu.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
NB Makala haya yametayarishwa na Mwanakwetu kwa heshima ya Mkufunzi Mtweve Kayanda kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Post a Comment