Adeladius Makwega-MBAGALA
“Tumaini la wanyonge, kwamba ipo serikali,
Ile nchi ya mazonge, ya wenye meno makali,
Wanyang'anyao matonge, wanyonge hawana hali,
Mwinyi ukiwa mkali, ndio raha ya raia?”
Msomaji wangu hilo ni mojawapo ya ubeti wa mashairi kutoka Diwani ya Chekacheka mashairi yaliyotungwa na Theobald Mvungi, kitabu hiki cha mashairi ni miongoni mwa vitabu alivyosoma Mwanakwetu akiwa mwanafunzi, ambapo siku ya leo amekikumbuka mno.
Siku ya leo msomaji wangi ni mwendo wa mashairi tu na unaweza kujiuliza Mwanakwetu anamfundisha msomaji wake kutunga na kughani mashairi? La hasha bali namna nyingine tu ya kuandika makala, msomaji wangu nakuomba upokea kwa heshima na taadhima shairi lingine ambalo limo katikahiyo hiyo Diwani ya Chekacheka hlii linaitwa Njiwa Kiumbe Mtini;
Nimejaribu Kujongea, yeye awe mkononi
Yeye juu hurukia , namuomba samahani
Nyimbo ananiimbia , nyimbo zachoma moyoni
Basi mie taabani, njiwa akitabasamu
Matawi nikiyakwea , njia ataruka kule
Si kwamba anikimbia , ni mbinu zake teule
Tabu huniongeza, hata chakula nisile
Njiwa Kushuska Hashuki na Mtini Haondoki
Majasho yananitoka , kwa imani nahamaki
Labda atatoweka au njiwa haondoki
Mvuto anaonioka , hatari ya kisa hiki
Njiwa kiumbe mtini, moyo waokwa mwilini
Unayoyafanya si kweli, njiwa acha tafurani
Moyo waunyima ari, kwa nini unauwini
Rudi usiende mbali , moyo uwe haueni
Njiwa ebu ubaini, moyo unavyoteseka.
Shairi la Njiwa Kiumbe Mtini limekumbukwa na Mwanakwetu juma lililopita la Mei 2025 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan kutoa maneno haya,
“Kama nilivyosema kwa sasa kuna maendeleo makubwa ya Tekinolojia, watu wanaweza kufanya wanavyotaka na watu wanaweza kutusema wanavyotaka, wanaweza kutoa matamko wanayotaka, niwaombe katika matamko yanayotoka ni vema Wizara na Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkajibu kwa haraka, mkachukua hatua za haraka, aidha kutoa ufafanuzi, kukanusha, au kama ni la kweli kukubaliana nalo na kuchukua hatua za kurekebisha, lakini tusiwe shamba la bibi, kila mtu anaweza kuja akafanya anavotaka kila mtu anaweza kuja Tanzania, watu wakajisemea tu.…pili tumeanza kuona, mtiririko na mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu, humu, sasa kama kwao wameshadhibitiwa, wasije kutuharibia huku.
Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi ambayo iliyobaki haijaharibika watu, wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, kuna majaribo kadhaa, niwaombe sana Vyombo vya Ulinzi na Usalama na nyinyi wasimamizi wa sera zetu nje, kutokutoa nafasi, kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja KUTOVUKA hapa, hapana.
Nimeona klipu kadhaa za kunisema, niko bias na nini, ninalolifanya ni kulinda nchi yangu na ndiyo wajibu niliyopewa. Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa KIUMBE yoyote kuja kutuvurugia hapa, awe yupo ndani au anatoka huko , hatutoi hiyo nafasi.”
Mwanakwetu kwa heshima zote alijiuliza je hii sentensi ya mwisho ilikuwa sahihi kwa matumizi ya lugha na kutumiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano ule?
“Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa KIUMBE yoyote, kuja kutuvurugia hapa, awe yupo ndani au anatoka huko hatutoi hiyo nafasi.”
Mwanakwetu kabla hajasema neno lolote anaomba atoe fasili ya neno KIUMBE.
“Mtu au mnyama au mdudu au ndege na vitu vingine vyenye uhai isipokuwa mimea.”
Neno KIUMBE linaweza kutumika na mwanadamu pale anapotaja mnyama ambaye siyo binadamu mathalani MBWA, SOKWE, PAKA , SIMBA, CHUI nk. Mathalani, Huyu Kiumbe amekula watu wengi na sasa tumemuuwa (Hapa wanakijiji wanarejea Mamba aliyekula watu kijijini.). Pia Neno KIUMBE linatumika na Mwenyeenzi Mungu pale anapomtaja mwanadamu mathalani,
“Adam na Hawa ni Viumbe wa mwenyeenzi Mungu, Mwanakwetu na Mwanahawa ni viumbe wa Mwenyenzi Mungu.”
Mungu anapotoa maagizo kwa mwanadamu katika vitabu vitakatifu kuna kuwa na lugha hii,
“Mwanadamu ni kiumbe changu nimekiumba kwa mfano wangu na pale kinapokengeuka nitakiadhibu.”
Mwanadamu kiungwana ananyimwa haki ya kumuita mwanadamu mwenzake KIUMBE na sentensi sahihi ilipaswa kuwa hii;
“Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa MTU yoyote kuja kutuvuruga hapa, awe ndani au kutoka nje hatutoi hiyo nafasi.”
Hilo juu ni la kwanza ambalo siku ya leo nimejaliwa kuliandika kwako msomaji wangu, sasa twende katika jambo la pili,
Katika makala kadhaa za Mwanakwetu huwa ninaeleza kuwa CCM ya sasa imekiuka Azimio nambali tatu la Kuundwa kwa chama hiki, ambalo ni Azimio la Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP lililofanyika Januari 21, 1977 yapo mambo matatu yaliyozungumzwa kwa pamoja baina ya TANU na ASP mojawapo ni kuvunjwa kwa TANU na ASP na jambo la pili lilikuwa vyama hivyo vinavyovunjwa siyo kwamba vimeshindwa kazi, bali wanaongeza nguvu ya pamoja na jambo la mwisho waliloazimia ni hili;
“Tumeamua Kwa pamoja kuunda chama kipya, kuendeleza Mapinduzi ya Kijamaa nchini Tanzania na Mapambano ya Ukombozi ya Bara zima la Afrika juu ya msingi iliyowekwa na TANU na ASP. Chama tunachounda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini na kupambana na jaribio lolote la mtu kumuonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya taifa.
Chama tunachounda tunataka kishike Barabara hatamu za uongozi wa shughuli zote za umma kwa maslahi ya Wakulima na Wafanyakazi wa taifa letu. Chama tunachokiunda tunataka kiwe kiungo kati ya Wanamapinduzi wa Tanzania na Wanamapinduzi wenzetu popote walipo.”
Hili likiwa azimo lililokuwa na maelezo ya kina kutoka kwa Wazee wa TANU na ASP ambapo Julius Kambarage Nyerere na Aboud Jumbe Mwinyi waliongoza kikao hicho. Kwa hakika kuendelea kutokea kwa matukio ya utekaji, udhalilishaji na mauwaji ya binadamu iwe kwa raia wa Tanzania au wageni katika ardhi ya Tanzania kupitia kinachoaminika kuwa ni watu wasiojulikana ni dhahiri vitendo hivyo ni uonevu kati ya binadamu na binadamu mwenzake, mtu mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi kama walivyosema Wazee wa TANU na ASP na walipinga tabia hizo kwa kauli moja na ndiyo maana hili likawa azimio lao.
Mpaka sasa masikitiko ya wengi matukio yanaendelea, wahusika hawakamatwi maswali yakiwa mengi; je hawa jamaa wanaofanya hivyo wanatumwa na nani? Watumia rasilimali zipi ? Nani mfadhili wake ? Je kama wanatumia silaha za moto zimetolewa na nani na je zinatokea wapi? Na je haya matukio yanatokea na kufanyika kwa faida ya nani? Kuendelea kwa matukio haya na kutokamatwa wahusika ni mkiuko wa azimio namba tatu baina ya TANU na ASP? Kwa hakika hilo sahihi ni mkiuko wa azimio namba tatu baina ya TANU na ASP la Januari 21, 1977.
Waliopaswa kulishughulikia hilo CCM lazima iwawajibishe mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kutoa nafasi ya CCM kujisafisha na kujitenga na kurudisha heshima kabla ya Watanzania hawajajongea katika sanduku la kura na vitendo hivyo vinavyomdhalilisha mwanadamu visiendelee.
Bila shaka msomaji wangu umeyatambua mambo yangu mawili katika makala haya; la kwanza ni lile la matumizi sahihi ya neno KIUMBE na la pili ni juu ya azimio namba tatu baina ya TANU na ASP la Januari 21, 1977.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu siku ya leo niliamua nitafakari nawe msomaji wangu juu ya mambo makubwa mawili kwanza juu ya matumizi sahihi ya neno KIUMBE na pili juu ya Azimio Nambali Tatu la TANU na ASP la Januari 21, 1977 na hayo yote mawili yanajadiliwa kulingana na hali kisiasa ya Tanzania mwaka huu wa 2025.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya niyaitaje? Azimio nambali tatu la TANU na ASP au Matumizi Sahihi ya Neno Kiumbe? Njiwa Kiumbe Mtini? Au Njiwa Kushuka Hashuki na Mtini Haondoki? Mwanakwetu anachagua Njiwa Kushuka Hashuki na Mtini Haondoki
Nakutakia Siku Njema
0717649257

Post a Comment