KILA MMOJA WETU ANAALIKWA KUWA YULE MWANAFUNZI MWINGINE-ASKOFU MLOGANZILA

 

Adeladius Makwega-Rorya MARA

Askofu Mabuga Mloganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma amesema kuwa Wakristo bado tupo katika Kipindi cha Pasaka, ambacho ni Kipindi Cha Ushuhuda, kinachoshuhudia ushindi wa Bwana Wetu Yesu Kristo dhidi ya Dhambi, dhidi ya Mauti , dhidi ya Dhuluma na dhidi ya kitu chochote Kibaya.

“Yesu anajitokeza mara kadhaa kwa wanafunzi wake, miongoni mwao wapo wanaomtambua na wapo ambao hawakumtambua kabisa. Petro hakumpokea Bwana Kwa kuwa alikuwa uchi, kwa mujibu wa mila za Kiyahudi kama umevaa nguo bila goti lako likaonekana wewe uuu uchi, hapa Petro hakuwa uchi wa mnyama, kwa hiyo Kasoro hiyo ya Petro ikasababisha hakumpokea Bwana.

Hata hivyo Yesu alimwambia Petro,’Ondoka mbele yangu wewe ni wa shetani.’ Petro alikuwa mtetezi wa Yesu hadharani lakini Yesu alimwambia Petro wewe utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.”

Haya yamesemwa Jumapili ya Tatu ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma ambapo Askofu Mlongazila alikuwa akitoa Kipaimara kwa vijana Wakatoliki mia mbili na ushehe, akihubiri katika Kanisa hilo lilojaa waamini wa Parokia ya Mwisenge alisema japokuwa Petro alimkana Yesu Mara tatu lakini baadaye alipewa jukumu la kulisha Kondoo wake.

“Hata katika maisha yetu sisi, kama binadamu tunao uzamani na usasa (upya). Hata Petro baadaye alikuwa mpya. Katika upya wa Petro alikuwa safi na kuendeleza kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa ungamo lake la dhambi.”

Kwa desturi Parokia ya Mwisenga huwa na misa tatu siku za dominika lakini Jumapili hii walikuwa na misa moja tu ya Kipaimara ambapo Baba Askofu Mloganzila aliiongoza, akiendelea na mahubiri yake Baba Askofu Mloganzila aligusia na hili,

“Leo tunatoa Sakramenti ya Kipaimara kwenu nyinyi vijana, katika imani yetu nyinyi mnakuwa imara Kiroho, maana yake Kanisa limeshawaaamini, japokuwa katika dunia hiii bado mnakaa kwa wazazi wenu na hata serikali haijawaruhusu kupiga kura na hata hamuwezi kupewa leseni ya kuendesha gari.

Hii nafasi inatolewa na kanisa kwetu sote, tuwe wanafunzi  bora wa Yesu. Vijana mna nafasi kubwa ya kumtambua Yesu, kumtetea na kumlinda na kuwafundisha vijana wenzenu habari za Yesu Kristo Mfufuka maana sasa vijana mnaingia katika mambo mengi mabaya.”

Akihubiri kwa lugha ya upole, taratibu, neno kwa neno, Baba Askofu Mabuga Mloganzila aliendelea kuwakumbusha vijana wa Kipaimara wajibu wao kwa kumfuata Kristo hadi kifo, aliongeza kuwa Injili Inadokeza kuwa Yesu alimpenda sana Yule Mwanafunzi Miwingine, hivyo basi Kanisa linatoa nafasi ya kila mmoja wetu kuwa Yule Mwanafunzi mwingine aliyependwa na Bwana Yesu. 

 


Askofu Mloganzila alisema kuwa Vijana wa Kipaimara wasiwe na aibu kwa kujifunza zaidi na wakitoka hapo wasiwe na aibu ya kumzungumzia Mungu na Kumkiri Yesu Kristo, wasiache kuongea juu ya Kristo, lazima wateseke kwa kutaka kuisha upya wao, maana sisi sote  ni wafuasi wa Kristo.

“Nyinyi tunawafinyanga kuwa watumishi katika Jumuiya ya Kristo , ni Maisha ya Kristo hadi kufa na ndiyo maana leo sote tumevaa nguo nyekundu, hatuwezi kunyamaza kumtetea Kristo hadi Kifo, kuiteta imani yetu, kuijua imani yetu na kuilinda imani yetu, tujitolea maisha yetu kama mchungaji mwema alivyo.”

Baba Askofu Mloganzila alisema kuwa rangi nyekundu inayovaliwa wakati wa Kipaimara maana yake ni kumwaga damu na hatuwezi kunyamaza katika hilo.

“Vijana someni alama za nyakati, someni mpate elimu, kuweni wanyenyekevu kwa viongozi na wazazi wenu, kuweni na macho na masikio yanayoona na kusikia alama hizo za nyakati, ujana ni nafasi ya kuandaa uzee wenu  ili muwe wazee wenye heshima.”

Baba Askofu Mloganzila pia aligusia tabia ya baadhi ya vijana kuachwa kwa tabia za kutumika vibaya katika mambo yasiyo ya msingi kisa fedha,  mathalani fujo na kushiriki mauwaji kisa pesa tu akisema hili siyo sahihi.

Ibada hii ya Misa ilimalizika majira ya mchana, huku vijana hao 200 na ushehe wakirudi majumbani mwao kwa sherehe hiyo ya Kipaimara ambacho ni miongoni mwa Sakramenti saba ndani ya Kanisa Katoliki.

SAKRAMENTI zipo saba (7), Nazo ni: 1. Ubatizo 2. Ekaristi Takatifu 3. Kipaimara 4. Mpako Mtakatifu 5. Kitubio 6. Daraja Takatifu 7.Ndoa. ambapo Mwanakwetu alipata Kipaimra mwaka 1993 Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es SalaamKipaimara hichi kilitolewa na Mwadhamu Kadinali Polcarp Pengo.”

Mwanakwetu kwa bahati mbaya japokuwa aliona kundi hilo kubwa la vijana waliopokea Sakrameni ya Kipaimara hapa Musoma Mjini lakini , lakini  na lakini kwa bahati mbaya hakupata mwaliko wowote ule. Mwanakwetu alirudi nyumbani kwake kinyonge na kupika ugali na dagaa wa Ziwa Victoria na kula , kisha kuyatayarisha makala haya na alipomaliza alikwenda kumtembelea rafiki yake wa utotoni Lukas Odoa huko Rorya ambaye alisoma naye Shule ya Msingi Mnazi Mmoja  Ilala Dar es Salaam  mwaka 1989.


 

Mwanakwetu upo?


 

Kumbuka

“Kila Mmoja Wetu Anaalikwa Kuwa Yule Mwanafunzi Mwingine.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257






 

0/Post a Comment/Comments