
Adeladius Makwega-SERENGETI –MARA
Ni majira ya asubuhi ya Mei 20, 2025 Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ikimbatana na wataalamu kadhaa kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mara, wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa huo ndugu Gerald Msabila Kusaya wanaanza safari kutoka Mjini Musoma kuelekea Wilaya ya Serengeti kukagua hali ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka wa 2020-2025.
Safari hii ilianza kwa mwendo wa kawaida wa kwenda umbali kama wa KM 30 gafla ya, la-haula wa la kwata, kwa bahati mbaya gari walilopanda wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara likapata pancha ya tairi ya nyuma mkono wa shoto, hapa hapa magari yote yaliyo katika msafara huo yalisimama na hivyo wataalamu watatu waliokuwa katika gari lililopata itilafu kuambiwa wapande katika gari la Katibu Tawala Mkoa wa Mara waendelee na safari, huku dereva na mtaalamu mmoja wakilifanyia matengenezo gari hili.
Kwa hakika umbali kutoka Musoma Mjini hadi Serengeti ni karibu KM 130, kwa hiyo pancha hiyo ilitokea hata robo ya safari ilikuwa bado, sasa wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ndani ya gari la Katibu Tawala wanaendelea na safari.
Wataalamu hawa wakiwa ndani ya gari la Katibu Tawala kulikuwa na mambo mazuri mengi, kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba nikusimulie kitu kimoja tu ambacho ni nyimbo zilizokuwa zinachezwa katika gari hii ya kiongozi huyu namba mbili katika Mkoa wa Mara akitanguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi.
“Nyimbo zote zilizochezwa tangu KM 30 hadi KM 130, ilikuwa miziki ya dansi ya bendi za Tanzania, miongoni mwao ni Kupenda Siyo Ndoto wa DDC Mlimani Park, Kata ya Maji Ukweni, Fatuma-Juwata Jazz Bend hizo ni sehemu tu ya nyimbo hizo kadhaa zilizochezwa garini.”
Kumbuka msomaji wangu anayekusimulia yumo kitini ndani ya gari hili, alipomtazama dereva wa gari la Katibu Tawala Mkoa wa Mara alikuwa kijana mdogo ambapo nyimbo zote hizo zilikuwa zimemzidi umri.
Hii miziki kwa hakika haifahamu vizuri lakini kuchezwa miziki hiyo ilionekana fika ni chaguo la Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ndugu Gerald Kusaya maana sauti za nyimbo hizo zilikuwa zinapishana kulingana na zilivyorekodiwa, hivyo Katibu Tawala mwenyewe alionekana akipunguza sauti kama wimbo ulikuwa na sauti kubwa na kuongeza sauti kama wimbo uliochezwa ulikuwa na sauti ndogo,
“Kama angekuwa hazipendi nyimbo hizo basi angezima, huku nyimbo hizo zilionekana zinachezwa katika flashi moja nyeupe.”
Tulipokuwa tunakaribia Serengeti Mjini wimbo wa Fatuma Maisha Ni Vita ndiyo unachezwa. Mwanakwetu akawa anaimba kimoyomoyo huu wimbo, huku akiufuatilizia neno kwa neno maana hawezi kuimba kwa sauti katika gari la kiongozi huyu maana huu usingalikuwa ustaarabu.
“Fatuma mimi nakwenda Nitarudiaaa, Fatuma ninakuomba uniombee duaaa, Jambo ninalokuomba Fatuma uchunge watoto na ujichunge na wewe ooooo Fatuma mamaa, Jambo ninalokuomba uchunge watoto na ujichunge na wewe ohhh Fatuma mamaaaa…Ukibadili tabia yako Fatuma jua nitambiwa nitaona vibaya tutatenganaaa….”
Wimbo huu unaimbwa, mara gari likafika Ofisi ya CCM ya Wilaya ya Serengeti na kufanyika kikao cha utambulisho ambapo Mwanakwetu alibaini kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara ilikuwa na wajumbe watatu; Mary Daniel, Marwa Mathayo na Mkuu wa Msafara huo Bi Rhobi Samweli.
Wajumbe hawa wa Kamati ya siasa CCM mkoa wa Mara katika wilaya ya Serengeti walikagua miradi mingi ikiwamo ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Bukome iliyojengwa kwa karibu shilingi milioni 380, ujenzi wa vyumba sita vya nadarasa katika Shule ya Sekondari Mapinduzi unaogarimu karibu shilingi milioni 150, Ujenzi wa Shule ya Msingi Muungano unaogarimu karibu shilingi milioni 540, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya sekondari Magumu unaogarimu karibu shilingi milioni 75.
Ukaguzi wa kila miradi hiyo ulifanyika kwanza kwa kupokea taarifa ya mradi, kisha kuukagua , alafu kusikiliza wananchi wanasema nini, kisha wajumbe wa Kamati ya Siasa kutoa maelekezo yao kwa serikali huku Katibu Tawala Mkoa wa Mara na wataalamu wake wakisikiliza kwa umakini mkubwa.
Kwa hakika Kamati ya siasa Mkoa wa Mara ilipokelewa vizuri katika Shule ya Msingi Muungano ambapo hamasa ilikuwa kubwa mno na jambo hilo kumvutia Kiongozi wa Msafara huo nayeye kutoa shilingi laki mbili kwa wanafunzi wa shule hii ya Msingi.
Kwa hakika viongozi wa wilaya nzima ya Serengeti tangu Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Katibu Tawala Wilaya , Afisa Elimu na Mganga Mkuu wa Wilaya na Baraza Zima wa Madiwani walipongezwa sana kwa uchapakazi wao.
Baada ya Kikao hicho msafara huu wa kamati ya Siasa ulianza safari kutoka Serengeti kuelekea Wilaya ya Bunda Vijijini.
Mwanakwetu upo
Kumbuka
“Kamati ya Siasa Mara Yaipongeza Wilaya ya Serengeti.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment