Adeladius Makwega Bunda MARA
Ni majira ya mchana ya Aprili 22, 2025 Mwanakwetu anaingia Wilayani Bunda akiwa katika gari aina ya Land Cruzer Hard Top nyeupe, ndani yake ikiwa na dazeni moja wa wanahabari na shabaha ni kuripoti tukio na ugeni wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ndiyo alikuwa anaingia mkoani Mara kwa ziara ya Siku tano , kipenga kikipigwa wilaya ya Bunda ambalo ni lango la mkoa wa Mara.
Macho ya Mwanakwetu yalimuona Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi akiwa amevalia suti yake ya rangi ya samawati iliyokoza, kichwani akiwa na kofia ya rangi hiyo iliyopachikwa picha ya Dkt. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mara masikio ya Mwanakwetu yalisikia wimbo wa Kapteni John Damiano Komba wa Harambeeee eee Harambe Mama Harambeee…
“Masikini ardhini wamelala watu…huu wimbo ya Kapteni John Komba hadi leo haujachuja...”
Haya meneno yanatamkwa na mwanahabari mmoja wa kike ambaye alikuwa kando ya Mwanakwetu. Wimbo uliendelea kuimbwa na mara Dkt. Emmanuel Nchimbi Katibu Mkuu wa CCM Taifa alisimama juu ya gari yake iliyokuwa mithili ya KIBANDA WAZI na kuwasalimu wananchi wa Wilaya ya Bunda. Kisha kutoa nafasi kwa watu kadhaa alioambatana nao akiwamo Mchungaji Peter Msigwa kuongea kwa kifupi.
“Chama Cha Mapinduzi kinajulikana kwa kufanya kazi iwe shuleni, hospitalini na hata usafiri wa anga huko kote unaziona kazi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi nimeungana na Jeshi kubwa la CCM ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama na maendeleo yanakwenda mbele na nchi yetu inapaa.
Mimi nimekuja kuwakatisha tamaa wapinzani, najua hapa wapo wapinzani, jamani huko upinzani mnapoteza muda, Tanzania ipo salama chini ya mikono ya CCM.”
Nayeye Mwenyekiti wa CCM mstaafu wa Wilaya ya Songea Mjini, Hamisi Abdalah Ally ilinadiwa kuwa ametumwa na Wazee wa Mkoa wa Ruvuma kuja na kijana wao Dkt Emmanuel Nchimbi,
“Jamani eeeh, kukaa na diwani, kukaa na Mbunge na pia kukaa Rais aliyemaliza muda wake ni kuisigina katiba, jamani eeeh lazima twende katika Uchaguzi Mkuu .”
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt. Nchimbi alizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bunda namna alivyofanya kazi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda na waalivyojenga shule za sekondari za kata 17 na vituo vya Afya kadhaa na namna alivyotatua mgogoro wa Nyatware hivi karibuni,
“Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi ni mtu makini, mtu mwema, najua anatoka JWTZ , Jeshi la Wananchi ni wakweli siyo watu waongo, hana maneno , yeye mwanajeshi mwenye utu na heshima kwa watu, Wananchi wa Mkoa wa Mara mumtumie vizuri MKUU WA MKOA WA MARA Kanali Mtambi mambo yatafanyika vizuri.”
Mwisho Katibu Mkuu wa CCM aliwaomba wananchi wa Bunda kuendelea kuiamini CCM na kushiriki zoezi la Uchaguzi Mkuu.
Katibu Mkuu Nchimbi alisema kuwa kutoiunga mkono CCM ni kosa kubwa ni sawa na kumuacha mke mzuri, mke mwema mliehangaika naye miaka mingi.
Mwanakwetu mwishoni alikusanya maoni ya wadau kadhaa waliokuwepo mkutanoni na wadau hao waliyasema haya,
“Maneno aliyoyasema, Katibu wa CCM Taifa ni mazuri, tunataka amani kisha mitano tena kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wanaccm wote tuendelee kushikamana na tufanye uchaguzi safi na kwa amani.”
Haya ni maoni ya Jumanne Magembe ambaye ni mwenyekiti wa CCM hapa Bunda.
Naye Khalifa Peter Kambaga Katibu wa CCM wa Kata ya Kabasa akayanadi haya;
“Nampongeza Katibu Mkuu wa CCM Taifa kwa kufanya ziara hapa Bunda, kwa kuwa ndipo alipoanza kazi kama Mkuu wa Wilaya, tunatoa ahadi kuwa hapa Bunda Dkt. Samia Suluhu Hassan atashinda kwa kishindo.”
Na yeye Daniel Yona Katibu wa CCM wa Tawi la Nyasala akisema haya,
“Napongeza tukio la leo kwa Katibu Mkuu CCM Taifa na mgombea mwenza kuongea nasi, sisi wanachama wa CCM tutatekeleza yote aliyoyasema na mama Samia mitano tena na sisi CCM tumeshamaliza uchaguzi.”
Katika maoni haya ambayo Mwanakwetu alikusanya akina mama na wao hawakuwa mbali wa kwanza alikuwa Nchaga Josefu Chale ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji, alisema kuwa Katibu Mkuu CCM taifa yupo vizuri wapinzani wawe kando na CCM iwe juu.
Maoni ya tano hapa Bunda yalikuwa ya Busilo Mnangasamo yeye alimuomba Katibu Mkuu CCM Taifa awasaidie wanakijiji wenzake kuezekewa jengo lao la Shule.
Nayeye Zuhura Makongoro Matutu alisema kuwa Katibu Mkuu Dkt . Nchimbi ameongea vizuri juu ya kuwa na amani hasa wakati wa uchaguzi, kila mmoja awe na nidhamu na tusifanye vurugu.
Kweli baada ya hutuba hiyo Dkt. Emmanuel Nchimbi aliingia garini na kuelekea Musoma Mjini kuendelea na ziara siku inayofuata Musoma.
Mwanakwetu upo?
Kwa hakika Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ni Bingwa wa kulitumia jukwaa vizuri na amezungumza vizuri, hata haya maoni ya watu sita waliongea na Mwanakwetu yanaeleza hilo.
Mwanakwetu akiwa Bunda alifanya Jitihada za kutafuta maoni ya wapinzani katika mkutano huo, lakini kwa bahati mbaya hakuna mtu aliyeweza kujitokeza hadharani kusema neno.
Baadaye Mwanakwetu akiwa amekata tamaa kabisa , kijana mmoja wa bodaboda akasema mzee hapa unaweza kuongea nini? Wakati Tundu Lissu yupo gerezani?
Kijana huyu aliposhawishiwa kuongea aligoma kisha akaiwasha bodaboda yake na kuondoka zake. Kwa hakika maelezo haya ya kijana wa Bodaboda yalimpa picha fulani Mwanakwetu juu ya kisa kimoja wakati akiwa mdogo ,kulikuwa na simulizi juu ya bondia Mmoja aliyepigana ngumi na bondia mwingine, huku bondia mwenye nguvu mkono wake mmoja ulifungwa minyororo.
Baadhi ya watoto wakati huo waliamini kuwa bondia huyu aliyekuwa anapigana na jamaa aliyefungwa minyororo ni Mohammed Ali, jamaa alipokuwa anapigana mambo yalikuwa magumu, bondia asiyefungwa minyororo alikuwa anashinda, jamaa akavunja sheria na kukata minyorororo na kisha kumchakaza mpinzani wake lakini jamaa hakupewa ushindi maana alikiuka sheria kwa kuikata minyororo.
Kwa hakika simulizi hii siyo ya kweli ni ya kubuni Mwanakwetu hafahamu aliyebuni ni nani na wengi wao wanalinganisha na lile pambano la Rumble In the jungle la mwaka 1974.
Ukweli wake ni huu.
“Katika mpambano wa masumbiwa ya kihistoria ya ‘Rumble in the Jungle’ mnamo Oktoba 30, 1974, Muhammad Ali alimshinda George Foreman huko Kinshasa, Zaire, na kutwaa tena taji la uzani wa juu la ndondi ulimwenguni.
Mohammed Ali alitumia mkakati wake wa kuegemea kamba na kumwacha Foreman achoke, hatimaye akamtoa nje katika raundi ya nane. Ushindi huu uliashiria mara ya pili kwa Mohammed Ali kama bingwa wa uzito wa juu na kuimarisha urithi wake kama mmoja wa mabondia wakubwa wa wakati wote.
Pambano hili lilifanyika Kinshasa, Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), mbele ya umati wa watu 60,000 na ilikuwa moja ya matukio yaliyotazamwa zaidi kwenye televisheni wakati huo.”
Mwanakwetu anachosema siku ya leo ni kuwa ukimsikiliza Dkt.Emmanuel Nchimbi na wote waliongea katika Mkutano wa hapa Bunda wanahitaja CHADEMA na Tundu Lissu, japokuwa muda mwingine hawaitaji moja kwa moja .
Tundu Lissu yupo katika minyororo gerezani, hapa hakuna kingine, hapa hakuna mwingine maana yake mpinzani wa kweli wa CCM kwa sasa ni CHADEMA chini ya Tundu Lissu.
Kuna wajibu mpambano huu kuwa huru ili kila mmoja asiwe minyororo ili kila mmoja atupe makonde yake yote, tuone mwisho wa siku itakuwaje?
Kwa hakika mpambano wa CCM na CHADEMA ni sawa na ule wa Mohammed Ally na George Foreman wa Rumble in the Jungle mwaka 1974.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka ,
“Watanzania Msimtaliki Mwanamke Mwema.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment