Adeladius Makwega-MARA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameanza ziara ya siku tano mkoani Mara Aprili 21, 2025 kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na za chama hicho tawala, hususani utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kipindi cha miaka tano tangu mwaka wa 2020 baada ya Uchaguzi Mkuu maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.
Mwanakwetu ameshuhudia wanachama wa CCM wakiwa na sare zao na magari yenye bendera ya chama hiki mitaani wakimngoja kiongozi huyu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Idara ya Siasa, Uenezi na Mafunzo ya CCM Mkoa wa Mara, Balozi Dkt. Nchimbi anatembelea wilaya za Bunda, Musoma, Butiama, Rorya, Tarime na Serengeti.
Hizo zikiwa wilaya zote za mkoa wa Mara, huku CCM mkoa Mara wakisema,
“Hii ni ziara ya kawaida kwa kiongozi huyo kujionea utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.”
Mwanakwetu amekuwa akijiuliza je ziara hii ya sasa mkoani Mara ya kiongozi huyu ina maana gani kwa CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2025 ?
“Huku nyuma ya pazia, Katibu Mkuu CCM ndiye mgombea mwenza akikokotana na mgombea Urais wa CCM wa sasa Dkt Samia Suluhu Hassan.”
Kwa utafiti wa Mwanakwetu Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi hajawahi kufika mkoani Mara kwa shughuli za kichama kama taarifa zinavyodokeza lakini,
“Balozi Dkt, Emmanuel Nchmbi alifika mkoani Mara, mara mbili, kwanza katika harusi na mara ya pili katika msiba wa mwanafamilia wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Mara Christopher Gachuma.”
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaona kuwa ,
“Kwa sasa CCM ina miezi mtano mbele kuelekea Uchaguzi Mkuu, mbele ya boksi la kura ili wapiga kura wafanye maamuzi, yaani mwezi Mei, Juni, Julai, Agosti na Septemba na pengine wapiga ramli za siasa wanasema kuwa shabaha ya Dkt. Emmanuel Nchimbi anapitia kuhakikisha anafukia mashimo ya Ilani ya CCM na kuweka sawa mambo ndani ya miezi hii mitano kuhakikisha mambo yanakaa sawa kama walivyotoa ahadi kwa wapiga kura mwaka wa 2020.”
Kwa hakika Mkoa wa Mara unafahamika wazi kuwa ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri wa madini, Mbuga ya Serengeti , Ziwa Victoria na ardhi yenye rutuba na tangu uhuru umekuwa ngome ya CCM maana ndipo alikozaliwa Mwalimu Julius Nyerere, lakini siasa za mkoa wa Mara zimekuwa tofauti, kwani hata huyu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara wa sasa Steven Wasira amewahi kuwa Mbunge kupitia Vyama vya Upinzani huku kukiwa na wabunge kadhaa wa upinzani wanaoshinda kila mara tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.
Mwanakwetu anaamini kuwa ziara hii ya Dkt. Nchimbi inaweza kutoa taswira halisi ya hali ya kisiasa ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 mkoani Mara hasa kwa namna Balozi Dkt. Nchimbi atakavyozungumza na wananchi, vikao vyake vya ndani na mwisho ni maoni ya wananchi baada ya ziara hii.
Mwanakwetu ana hakika atafanya uchambuzi mzuri baada ya ziara hii kukamilika.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
Ujio wa Katibu Mkuu CCM Taifa Mkoani Mara Una Maana Gani?
Nakutakia siku njema
0717649257
Post a Comment