UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2025 MGUMU

 



Adeladius Makwega-MBAGALA

Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi wa katuni, ambapo mtayarishaji wa makala haya huchagua katuni nne kutoka vyanzo kadhaa na kisha kuzielezea namna zilivyochora kisha kuzichambua kwa jicho la mtayarishaji.

Kuyaanza makala haya Mwanakwetu ameikamata katuni ya kwanza ilivyochorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani ambapo kunaonekana kuna mandhari mbili, moja ya mjini na moja ya kijijini wakati wa msimu wa mvua kubwa. Mandhari ya Kijijini kunaonekana jamaa wapo shambani wanalima wakisema huu ni msimu wa Baraka, mvua ikiendelea hivi tutavuna sana na mazao haya hayakauki tena.Mandhari ya mjini kunaoneka jamaa na wao wakiyasema yao; Huu ni msimu wa tabu, mvua ikiendelea hivi biashara hatuwezi kufanya kabisa, sababu hakuna wateja na hapa jamaa wengine wa mjini wanasema hii mvua sijui tutafikaje nyumbani kwetu?


 

Kwa hakika huo ndiyo ubinadamu na ndiyo maana wasanii wengi wameimba juu ya mvua na jua mwanadamu anapenda nini? Kikubwa mwanadamu kwa namna alivyo ni vigumu kuridhika na hali yoyote ile na huo ndiyo ubinadamu ulivyo.

Mwanakwetu anaiweka kando katuni hii na kuikamata katuni ya pili ambayo pia imechorwa na Said wa Michael, yule yule wa DW KISWAHILi hapa kunaonekana jamaa kadhaa wamekamatwa na kitu kinachoitwa uhaini na hawa ni wanasiasa wa upinzani katika mataifa kadhaa ya Afrika likiwamo Tanzania, maana anaonekana ndugu yetu Tundu Lissu akiwa kakabwa katika sekeseke hili. Kwa hakika katuni hii ilipotazamwa na Mwanakwetu akilini mwake alikuja na swali,

“Inakuwaje kesi za uhaini kichaka chake ni Bara la Afrika? Lakini Ulaya na Marekani hali imekuwa tofauti.”

Jibu lake ni hili,

“Kesi za uhaini hazipatikani mara kwa mara barani Ulaya leo hii hasa kwa sababu ya mchanganyiko wa mambo, ikiwa ni pamoja na mageuzi ya mifumo ya kisheria na siasa zake, kuzingatia vitisho vya kisiasa kama vile ugaidi, na kukomeshwa kwa adhabu ya kifo katika nchi nyingi za Ulaya. Zaidi ya hayo, makosa mbadala ya jinai mara nyingi huchukuliwa kuwa yanafaa zaidi katika kushughulikia hatua ambazo zingeweza kushitakiwa hapo awali kama uhaini lakini mahusiano ya Kidugu baina ya vyama vya siasa na kuacha siasa za visa , chuki, uhasama na wizi wa kura kutotiliwa mkazo sana. Vita vikubwa vimekuwa vya uchumi wa mataifa yao.”

 

Mwanakwetu anaamini kuwa hata nia ya Mhariri wa Propaganda wa DW KISWAHILI ya kuipachika katuni hii ni kutunanga waAfrika kuachana na vita vya kisiasa, tuwe na vita vya kiuchumi na maadui wa vita vya uchumi hawewezi kuwa ndani ya Ardhi yako bali mataifa mengine. Mhariri wa DW KISWAHILI anapingana na dhana ya mashauri ya uhaini kwa wanasiasa wa Afrika kupewa kesi za uhaini.Huku historia inadokeza kuwa Mwingereza wa mwisho kunyongwa kwa uhaini alikuwa ni ndugu Wiliam James ambaye alinyongwa mwaka 1946 kosa alilotiwa hatiani ni kufanya propaganda za chama cha NAZI na huku shauri la mwisho la uhaini kwa Uingereza lilikuwa dhidi ya Jaswant Singh Chail ambaye alihukumuwa miaka tisa jela mwaka 2023 kwa tuhuma za kutaka kumuua Malkia Elizabeth enzi za uhai wake.


 

 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu ambayo imechorwa Godfrey Mwampembwa maarufu kama GADO ambaye ni mzaliwa wa Tanzania ambye anafanya kazi zake huko nchini Kenya na magazeti kadhaa, GADO alizaliwa Agosti 6, 1969 sasa akiwa na umri wa miaka 56. Gado akihojiwa na la gazeti la Financial Times la Uingereza juu na uchoraji wake wa Katuni alisema kuwa anachora sana katuni zenye maudhui ya viongozi wa Afrika ambapo hilo ni ndiyo shida kubwa ya Afrika ya leo.


 

 

Mwanakwetu katika makala haya anazo katuni mbili za GADO moja inamuonesha mama mmoja yupo mezani akiwa na umma, kisu , kijiko na mbele yako kuna nyama ya ndafu na imepewa jina Uchaguzi Mkuu wa 2025 nchini Tanzania, katuni hii kwa kuitazama vizuri sura ya mama huyu ni kama ya Dkt Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akijiandaa kwa uchaguzi huo. Katuni hii inadokeza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025 utakuwa mwepesi kwa Rais Samia ambalo litakuwa sawa na kula nyama ya ndafu katika karamu maalumu ambapo hilo Mwanakwetu anapingana nalo 100 kwa 100 maana hali ya uchaguzi itakuwa ngumu mno siyo kwa Rais Samia mwenyewe tu bali hata kwa chama chake chake CCM maana mwaka 2025 akili za wapiga kura zilihitaji CCM kuja jina jipya la mgombea urais, lakini pia Rais Samia tayari ameshafanya kazi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha miaka inayokaribia mine kwa hiyo wapiga kura wameshampima mgombea huyu wa CCM kwa chungu na tamu zake.


 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya nne ya GADO ambayo inaonesha watu wawili mwanamake na mwanaume wapo kando ya kaburi. Huyu Mwanamke ni kama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwanaume kando ni kama  Dkt Jakaya Kikwete Rais Mstaafu wa Awamu ya nne akiwa amemshikia kandili Rais Samia akisoma kitu kando ya kaburi, kaburi hilo limepewa jina John Pombe Magufuli Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa inavyoonekana kwa mujibu wa kabila wa Wapogolo kinachofanyika hapa na Samia na Jakaya kana kwamba WANAPETAMASHI (WANATAMBIKA) kuona kwamba mambo yatakuwaje wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kipi kifanyike? Kaburi la John Pombe Magufuli linasema maneno haya,

“Sasa nimevutiwa sana na namna mambo yanavyokwenda lakini juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 lazima ukabe shingo kweli kweli.”

Kwa hakika mchroaji wa katuni namna alivyomchora Dkt. Jakaya Kikwete amesmshkia kandili Dkt Samia hiyo ndiyo halisi ya mahusiana ya karibu kwa sasa baina ya viongozi hawa tangu uteuzi wa Dkt. Samia kuchaguliwa kupeperusha bendera ya CCM. Ujirani huo unao faida lakini wakati huo hup zipo hasara tele , hasara mojawapo ni wapiga kuwa wanaweza kupiga kuwa kwa kushindwa kumtafuatisha Dkt Samia mwenyewe na huyu mshika kandili Dkt Jakaya Kikwete lakini hizo ndizo siasa ngoja tuone mwisho utakuwaje?

Mwanakwetu hana cha kuongeza katika katuni hii.

 


Basi hadi hapo ndiyo ninatia nanga ya makala ya katuni siku ya leo, kumbuka Mwanakwetu alikuwa na katuni nne zile mbili za Saidi wa Michaeli moja ya hali ya hewa na mzingira ya mjini na kijijini nayo katuni ya pili ni juu ya mashtaka ya uhaini barani Afrika. Katuni ya tatu na nne zote ni GADO ambazo zinazungumzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025. Kwa katuni hizo nne ndiyo zinalianua jamvi la makala ya katuni siku ya leo.

Kumbuka,

“UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2025 MGUMU.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257








 

 

0/Post a Comment/Comments