Adeladius Makwega-MBAGALA
Mei 24, 2022 nilishuka katika basi linalotokea Mji wa Serikali Jijini Dodona kuelekea nyumbani kwangu, nilipiga hatua kadhaa, mara nikasikia kishindo nyuma yangu, nikageuka kuona kulikoni? Nilimuona mama wa makamo nyuma yangu aliyevalia blauzi nyeupe, Khanga nyekundu, viatu aina laba akiwa amesuka nne kichwa, kitembea kwa kunifuatilia namna ninavyotembea.
Akanisalimu kwa Kigogo Mianyenyi–Misaaa (nikajibu).
Akaniambia kwa Kiswahili nimependa hatua zako unavyotembea kwa mwendo wa haraka, Mwanakwetu nikastajabu moyoni kisha nikacheka, mama kahusudu miondoko ya Mwanakwetu, nikasema moyoni mama hii miondoko hauiwezi, hizi ni freekwenshi nyingine kabisa, freekwensi hizi ni za akina Julius Kambarege, haya niyasema moyoni tu.kisha nikamjibu sawa mama, hakuna neno.
Nikamuuliza mama wewe unakwenda wapi? Akanjibu kuwa yeye anakwenda Chamwino Sekondari ana binti yake anasoma kidato cha kwanza na yu mgonjwa anakwenda kumuona.
Msomaji wangu nakuomba nikwambie kitu, Mwanakwetu kwa namna nilivyo, Wagogo ni kabila la mama zangu huwa hata wanawake wa Kigogo nikutana nao huwa huwa siwatanii hata mara moja nawapa heshima zao za umama bila ya wao wenyewe kufahamu, mara zote huwa sivuki mipaka hata ya utani nao.
Kiungwana mama huyu anayekwenda kumuona bintiye nikampa pole, akanijibu asante.
Nikamuuliza mbona muda huu ni jioni, kwanini hukudamka mapema? Mama huyu akanijibu kuwa yeye anaishi Ihumwa na kazi yake kubwa ni mkulima wa mbogaboga, kwa hiyo hudamka asubuhi sana huenda bustanini kwake kumwagilia, kwa hiyo atoke huko, arudi nyumbani, apike, alafu anapomaliza ndipo safari za kwa ndugu na majirani na wagonjwa zinaanza.
Nikampa hongera kwa kazi, akajibu asante.
Nikamuuliza sasa mbona unakwenda mwenyewe mzee umemuacha wapi? Mama huyu ambaye alinifahamisha jina lake ni Mdala Rehema akanjibu kuwa mumewe ni bingwa Ujimbi(Pombe) na muda huu hawezi kumkamata kabisa maana yupo ulevini.
“Saa hizi ni mida yake ya kupepesuka tu hadi saa nne ya usiku ndiyo anarudi nyumbani.”
Wakati mama huyu anasema hayo alikuwa akiigiza kupepesuka anaongea kwa vitendo sana. Mama huyu nikampenda maana ni watu wachache ambao huongea maneno na vitendo kwa sambamba , hiyo karama lakini wapo ambao ni wasanii wa Muziki , Kwaya za Kanisani Ngoma za Asili kama mtu alianza kucheza hizo Kwaya mapema kuimba kwa vitendo kunaweza kuhamia hata kuongea kwa vitendo.
Nikuuulize msomaji wangu wewe unapongea unaongea kwa vitendo? Natambua Jibu lako unalo je umeshakutana na mtu ambaye hamalizl sentensi baada ya kuongea na kuichanganyia na vitendo? Najua na hili jibu unalo.
Mama huyu akaniuliza na wewe huku unakwenda wapi? Nikamjibu kuwa nakwenda nyumbani kwangu mama, mama huyu akawa anasema.
“Baba mimi naishika dini yangu sana sana, lakini wanaume wa kwetu dini inawashinda kabisa kwa mambo makubwa mawili nayo ni Wadala (wanawake) na Ujimbi (pombe ) tu. Hiyo ndiyo Misalaba ya Wanaume wa Kigogo Mimi baba nashika dini sana.”
Nikamwambia mama huyu kuwa mwombee rehema za Mungu zimtembelee mumeo ili aweze kuepukana na mambo hayo mawili, akajibu kuwa anafanya hivyo kila siku.
Mle njiani watu wanashanga huyu jirani yetu(Mwanakwetu ) Huyu mwanamke anayeongea naye kampata wapi? Wanasema kwa kuniteta kwa Kigogo,
“Jirani kapata Mdala.”
Kigogp ni lugha ya mama naisikia vizuri japokuwa kuongea ni Bahati Nasibu, huyu mama niliyenaye kando ananiambia majirani zako wanasema jirani yao leo umeopoa demu.
Nikamwmabia mama huyu kuwa hata wewe na mumeo, unaweza kudhani mumeo kila wakati yeye na wadala baa kumbe hamna lolote, saa zingine mambo kama haya. Mama huyu akasema kweli baba!NIkamjibu Ndiyo nakwammbi ndiyo. Kisha akasema,
“Wanaume wa Kigogo wanakwenda kwenye ujimbi huko huko wanakutana na wadala, wanaokunywa nao, hapo hapo na mambo yote yanamalizikia huko huko, na siye tuliobakia nyumbani mambo ya kwetu hayapo tena. Mimi baba ni nyumbani, Kanisani, mazoezi ya Kwaya Kanisani ,Bustanini na kutembelea ndugu basi.”
Nikamwambia mama huyu Hongera sana , kisha akaongeza maneno haya,
“Sasa hao wanawake wenyewe wa baa wangekuwa mabinti wadogo! Aha wapi wazee wenzetu, wanaume mnahangaika na nini?.”
Nikamuuliza kweli mama? Akajibu kweli kabisa baba, sasa sijui kwetu wamekosa nini? Nikacheka alafu nikamwambia,
“Mama kipo walichokikosa, maana hao hao wazee wenzako ndiyo wanaojua kupika vizuri, kuliko hata mabinti wadogo wadogo, yatathimini mapishi yako, kisha usiwe unamsema sana ukiwa naye, punguza maneno kuwa mtu wa vitendo pengine anakimbia gubu. Wao wanajua kupika na kuunga vizuri sana na pengine wewe nyumbani unapika chukuchuku tu.”
Nilimuuma sikio.
Mama huyu akacheka sana kasha akasema mtu akajitokea katika pombe zake hata upike na uunge na karanga na samli au nazi unafikiri ataweza kula ?
Nikacheka sana, kisha mama huyu akaendelea,
“Hata kutambua kama chakula kinaonga! Hawezi tambua. Raha ya kula mtu awe hajalewa atajilaba hadi vidole.”
Alisema Mdala Rehema.
Nikacheka sana, nikamuuaga nikachepuka njia ya kuelekea kwangu na mdala Rehema kuelekea Shule ya sekondari Chamwino kumuona bintiye mgonjwa.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kikubwa ni malalamiko ya mdala Rehema juu ya wanaume wa Kigogo ambao ni wajomba wa Mwanakwetu kuwa wanapemba pombe na wanawake, wajomba zangu pimeni kisha kama lipo la kufanyia kazi basi lifanyiwe.
Mdala Rehema anasema Ujimbi na Wadala ni Msalaba wa Wanaume wa Kigogo je huo ni msalaba wa wanaume Tanzania.
Mwanakwetu upo ?
Kumbuka
“Msalaba wa Wanaume wa Kigogo.”
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment