Adeladius Makwega-MWANZA
Msomaji wangu, leo ni siku nyingine, wakati mwingine wakukualika katika kuzichagua, kuzielezea na kuzichambua katuni nne ndani ya makala ya katuni.
Kumbuka haya ni makala ya uchambuzi yakiongozwa na katuni hizo. Kwa kuyaanza makala haya ninaikamata katuni inayoonesha mazingira ya darasani huku wanafunzi wakisimamiwa mtihani, katika chumba hiki cha darasa kunaoneka wanafunzi wawili, wa mbele amegeuza shingo anatizamia majibu kwa mwanafunzi wa nyuma yake.
Mabegi ya wanafunzi hawa yapo chini sakafuni lakini yamepewa utambulisho wa ramani mbili, wa nyuma ni ramani ya Tanzania na wa mbele mpiga chabo ramani ya Uganda. Ndiyo kusema Uganda anatizama majibu kwa Tanzania, Mtihani huo umepewa jina COVID TEST.
Mwanakwetu anapoizama tena na tena katuni hii amebaini kuwa ilichorwa wakati wa Ugonjwa wa Korona ambapo mataifa jirani yaliiga mengi kutoka Tanzania kutokana na msimamo usiyoyumba wa Rais John Pombe Magufuli akiwa hai na kwa hakika huyu mwanafunzi mwenye bendera ya Tanzania anafanana fika na marehemu Magufuli. Kwa hakika wapo waliyopinga msimamo huo lakini kubwa John Magufuli alitimiza wajibu wake kama kiongozi na kuvuka katika ugonjwa huo. Dhana hii ya COVID TEST inaweza kuwa jambo lolote ambalo linalitea taifa changamoto, kikubwa kupatiwa ufumbuzi huku tukiwa mfano kwa majirani zetu. Viongozi wetu wafanye kazi kwa bidii.
Sasa nakutana na katuni nyengine ambayo inanipa nafasi ya kukutana na maudhui mengine, kunaonekana binadamu wawili na wanyama kadhaa, hawa binadamu, mmoja kavaa sare kama za askari wa wanyama pori wa Tanzania, ana kirungu huku akisema, kaa mbali na hawa wanyama, huyu jamaa kando ni kama Mmaasai. Juu ya picha hii kuna maneno haya, Wamaasai wa Tanzania wamefurushwa kutoka eneo lao la mababu na mababu. Wanyama kando na wao wanavunja ukimya wanasema, mbona jamani binadamu hamkutuomba maoni yetu mapema ? Hapa kana kwamba wanyama hao wanasikitishwa na hili jambo. Kwa hakika hapa mchoraji wa katuni hii anawapa sifa za binadamu wanyama hao akiwamo Twiga, Tembo na wanyama wengine na kibaya hakuna binadamu mwingine anayeonekana kusema lolote tena.
Mwanakwetu anapoitazama katuni hii na tukio hilo, huku akiwa amepitia maoni mengi yakiwamo yanayoonesha kuwa Rais Samia ndiye kiongozi pekee ambaye anaweza kuiokoa au kuizamisha jamii ya Wamaasai ambayo bado inaheshimu na kutunza utamaduni wake hadi kesho. Matumaini haya hasi na chanya kwa Rais Samia yakiwa kando na yakichorwa katika katuni ya tatu inayoonesha sura kadhaa za Rais Samia kwa jamii ya Wamaasai, je Rais Samia ataonesha sura gani?
Mwanakwetu katika hili linalomuongoza na maudhui ya katuni yake anajiuliza na kuyakumbuka mengi, huku wengine wakiwananga kuwa Wamaasai hao ni kutoka Kenya , kweli jamani tumefikia hapo?
Je itakuwa sahihi jamii hii ikaagushe machozi yao katika kaburi la Sokoine na lile la Profesa Saitoti?
“Jamii za Maasai wa Kenya na Tanzania ni jamii ile ile, zimewahi kuwa na viongozi wakubwa na makini sana katika Serikali ya Kenya na Serikali ya Tanzania, akiwamo marehemu Profesa George Saitoti-Kenya, marehemu Edward Moringe Sokoine.-Tanzania.”
Swali ni Je Profesa Saitoti na Sokoine Wangekubaliana na hili linalofanyika sasa kwa jamii yao miaka kadhaa baada mkoloni kwenda zake? Labda msomaji wangu nikukumbushe tu,.
“Edward Sokoine angekuwa na miaka 86 kama angekuwa hai hadi leo hii; Profesa George Saitoti angekuwa na miaka 79 kama angekuwa hai hadi leo. Moringe alizaliwa Agosti 1,1938 naye Saitoti alizaliwa Agosti 3, 1945. Moringe aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa nyakati mbili tofauti naye Profesa Saitoto aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Kenya.Huko Profesa Saitoti alifariki katika ajali ya hedikopta Juni 10, 2012 naye Sokoine alifariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984.”
Kama hao ndugu wangekuwa hai kwa hakika wangekuwa ni miongoni mwa Wazee wa mataifa yetu.
Mwanakwetu anaamini haya,
“Kwa hakika Edward Moringe na Profesa George Saitoti wangekuwa hai wangekubaliana na maendeleo kadhaa ambaye jamii ya Wamaasai na jamii zote za wafugaji waliyoyafikia sasa, mathalani upatikanaji wa elimu na kuongezeka kwa watoto wa jamii za wafugaji kuwa wajuzi wa taaluma mbalimbali kama vile Wanasheria, Matabibu, Wauguzi, Walimu, Maprofesa, Mainjinia na kadhalika lakini kwa hakika wasingekubaliana kabisa na hamisha hamisha ya ndugu zao toka eneo moja kwenda lingine. Nazo shutuma za ubaguzi za kusema hawa Wakenya hawa si Watanzania zikiwasindikiza, Ikumbukwe kuwa kabia lolote linaheshimu kwanza kabila lake alafu ndipo utaifa unafuata. Katika hili linahitaji umakini mkubwa kuliendea.”
Sokoine na Saitoti wakiwa hai walipambania kwanza heshima ya kabila lao, walipambania upatikanaji wa dawa za mifugo, walipambania maeneo ya kuchungia na kupatikana kwa huduma muhimu kwa jamii zao kama vile elimu na tiba ambazo awali zilitolewa wa watu makabila mengine. Hali hii iliongeza idadi ya watoto wa wafugaji kuingia vyuo vikuu na kuwa wanataaluma mbalimbali kwa Kenya na Tanzania huku wakiendeleza ufugaji ambayo ni kazi yao ya asili.
Mwanakwetu anasema kutolifanyia kazi suala la Wamaasai ni kuruhusu jamii hii kuyaangusha machozi katika makaburi ya Sokoine na Profesa Saitoti. Hatupaswi kulipa Kisogo jambo hili, lazima litatuliwe kwa wakati na jamii hii ili iendelee na shughuli zake za maendeleo.
Sasa nakutana na katuni ya nne ambayo inaonesha mandhari ya kupiga kura ambapo wapiga kura wapo katika chumba hicho wanapiga kura katika masanduku kadhaa, haya masanduku kila moja lina maneno, chumba hiki yupo jamaa anayesimamia zoezi hili na mpiga kura mmoja amepiga kura yake vizuri, sasa anatoka nje lakini juu ya mlango wa chumba hicho kuna maneno haya ukishapiga kura alafu kipi? Yaani kinafuata nini?Mwanakwetu anapoitazama katuni hii anaona kuwa kupiga kura hakuna maana kama mambo yataendelea kufanyika vile vile, wajibu kwa wanaochaguliwa ni kutekeleza yale waliyotoa ahadi kwa wananchi, vinginevyo hilo linaweza kuwakatisha tamaa wananchi na umuhimu wa kupiga kura usionekane.
Mwanakwetu Upo?
Basi hadi hapo msomaji wangu ndiyo nimekamilisha uchambuzi huu wa makala ya katuni siku ya leo. Nilikuwa na katuni nne, ile ya jamaa anayeangalizia darasani, ile ya hamisha hamisha ya jamii ya Wamaasai ya tatu ni ile ya sura kadhaa za Rais Samia na ya nne ni hii ya kupiga kura, ndiyo na mimi naufunga huu ukurasa wa makala ya katuni siku ya leo.
Kumbuka,
“MACHOZI KABURI LA SAKOINE NA SAITOTI.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment