Adeladius Makwega-MWANZA
Mwishoni mwa wiki ya Mei 12, 2022 Mwanakweti alikuwa
anajiandaa na safari ya kwenda Tanga, alipokuwa anatafuta zawadi za kwenda nazo
huko kwa ajili ya familia yake, alibaini kuwa japokuwa Tanga wana matunda mengi
lakini ubuyu haupo. Kwa hiyo alimuagiza kijana mmoja wa Chigogo amletee gunia
la ubuyu ili kuweza kwenda nao huko.
Kweli aliletewa gunia zima la ubuyu kwa shilingi
15,000/-huku likiwa limeja pomoni, akaliangalia vizuri lile gunia akasema ni
mzigo mkubwa mno kusafiri nao hadi Tanga. Akafikiriii alfau akasema,
“ Niende mashine jirani na kuwaeleza waupitishe katika mashine ya
kukoboa ili nipate unga wake tu na mzigo uwe mwepesi.”
Alifanya hivyo na kupata madebe mawili ya unga wa
ubuyu, alipomaliza kazi hiyo akaona mbegu za ubuyu nyingi katika madebe zaidi
ya manne.
Akauliza,
“Sasa hizi mbegu zinatupwa?”
Kijana wa mashine akajibu,
“Ndiyo, zinatupwa mzee, lakini zamani tulikuwa tunazikamua mafuta au
tunasaga katika jiwe/kinu na kuwa kiungo kizuri sana kwa mboga za Wagogo na
wengine wakifanya baishara ya unga huo wa mbegu za ubuyu na mafuta yake.Kwa
bahati mbaya Serikali ikapiga marufuku, wakisema mafuta ya ubuyu yana madhara
kiafya.”
Nikamwambia kijana wa mashine nifungie mbegu zangu,
nikawekewa katika kiroba na kwenda nazo kwangu. Kijana aliyebeba akauliza mzee
hizi unakwenda nazo wapi? nikamwambia nyumbani kwangu kuna bonde kwa hiyo hizi
mbegu naenda kuzimwaga hapo kupunguza mmomonyoko wa udongo katika bonde hilo.
“Mzee zitaota hizi, maana ardhi ya Dodoma ni udongo wa mibuyu.”
Nikajibu kuwa ikiwa inaota nitakuwa naipunguza
kidogo kidogo.
Mzee, hizi mbegu zamani ilikuwa pesa ya maana sana,
hata jirani yako alikuwa ni miongoni wa wafanyabiashara wa mafuta ya ubuyu,
alisema kijana huyu.
“Mbegu za ubuyu kwa Dodoma, Singida na mikoa mingi jirani zinapatikana
kwa wingi kama zingetumika sana zingeua kabisa soko la mafuta ya madukani na
sisi Wagogo ni kiungo chetu cha miaka mingi hasa hasa zile mbegu zikitwangwa
katika kinu na kuungia mboga zetu, mboga inanoga sana.”
Aliniambia kijana aliyenibebea mizigo, huku
nikimtambua kwa jina moja la Josefu.
Nikashushiwa mizigo yangu na kwenda hadi kwa
jirani, Nilipiga hodi na kukaribishwa vizuri, nikamuuliza eti jirani uliwahi
kufanya biashara ya mafuta ya ubuyu?
Mama huyu anayefahamika kama Mdala Zipora alinjibu
kuwa mwanangu biashara hiyo ilishamiri mno wakati wa Urais wa Jakaya Kikwete na
lita moja ya mafuta ya ubuyu yalikuwa kati ya shilingi 20,000-30,000/-
Hivi sasa kuna shida ya mafuta, mimi wala
nisingepata tabu, ningekusanya mbegu zangu na kukamua mafuta hayo, ningepata
pesa na ningepata mafuta ya kupikia. Alisema jirani yangu huyu ambaye ni mama
mwenye umri kati ya miaka 63-65.
Binafsi nikasema kama kwa mwaka 2013 lita moja
iliuzwa shlingi 30,000/- miaka 10 sasa lita moja ingefika zaidi ya shilingi
50,000/- ambayo ni mara 16 ya lita ya petrol kwa bei ya sasa na pia ni mara
tano ya bei ya lita moja ya asali ya nyuki wakubwa kwa sasa inayouzwa shilingi
10,000/-
Msomaji wangu hiyo nakisi ya bei ya lita moja ya
mafuta ya ubuyu kwa lita moja asali au petrol inakupa picha ya thamani ya
mafuta hayo.
Lakini Serikali Ikatangaza mafuta hayo yana madhara
kiafya hivyo yasitumike kabisa.
“Hapa Dodoma palikuwa na Mkorea ambaye alikuwa akinunua unga wa ubuyu na
mbegu zake ambazo alizikamua na kuyachukua mafuta hayo na mimi nilikuwa naenda
kukamua na kuyauza kwa wateja wangu wengi yaani baba! Hata ukikamua robo ya
lita unauza kwa shilingi kati ya 6,000-7,000/-.”
Alisema Mdala Zipora.
Kwa kuwa Jakaya Kikwete alikuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 2005-2015,binafsi nikaanza kutafuta taarifa
za mafuta ya ubuyu katika kipindi hicho juu ya katazo hilo na athari zake
kiafya.
Kulingana na taarifa iliyoandikwa na mwanahabari
Theopista Nsanzungwako ya Julai 8, 2013 katika gazeti la serikali Habari Leo
ilisema kuwa,
“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la Wajasiriamali wanaouza mafuta ya
ubuyu kama dawa, na kuwaelekeza wananchi kunywa, napenda kuwataarifu kuwa
mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta.”
Gazeti hilo lilimnukuu msemaji wa TFDA Gaudensia
Simwanza aliyekuwepo katika maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa Dar es
Salaam huku msako ulifanyika katika maonesho hayo kwa wale waliodiriki kufanya
biashara hiyo hapo kiwanjani.
Jambo hilo halikuishia hapo nalo Gazeti la
Mwananchi la Julai 31, 2013, siku 23 baada ya TFDA kusema hayo, lilimnukuu Mkemia
Mkuu wa Serikali wakati huo, Profesa Samwel Manyele akiwataka Watanzania kuacha
kutumia mafuta ya ubuyu kwa maelezo kuwa yana kemikali yenye madhara kwa afya
ya binadamu.
Profesa Manyele alipinga kauli iliyotolewa na
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwanzoni mwa wiki hiyo wakati huo kwamba
mafuta hayo hayana madhara katika mwili wa binadamu yakitumiwa vizuri.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wakati huo,
Dk Seif Rashid, alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa huo
ndiyo msimamo wa serikali kuhusu mafuta hayo, hivyo wananchi waamue wenyewe
kuyatumia au kutokuyatumia.
Akizungumza na gazeti mwananchi, Profesa Manyele
alisema,
“Ofisi yangu inaiunga mkono kauli ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini
(TFDA) kuzuia matumizi ya mafuta hayo, Watanzania wanatakiwa kuwa wasikivu na
onyo hilo.”
Alisema sheria inayoruhusu mtu yoyote kufanya
biashara ya chakula na dawa ipo chini ya TFDA, wao ndio wanaotoa kibali cha
kufanya biashara na kutengeneza bidhaa, kwamba wakisema bidhaa fulani haifai
wanatakiwa kusikilizwa.
“Wao ndio wanaotoa kibali cha kutengeneza bidhaa, pia wana uwezo wa
kuzuia uzalishaji kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Mkemia Mkuu haiwezi kuzuia
uzalishaji.”
Aliongeza kuwa tayari TFDA imeshaeleza athari ya
kemikali iliyopo katika mafuta ya ubuyu inayoweza kuathiri afya za Watanzania,
kuwataka wananchi kuwa makini na kama wanahitaji taarifa za msingi wanatakiwa
kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo.
“Mimi kama Mkemia Mkuu wa Serikali nitaingilia kati kama mambo yote
yatashindikana na serikali itataka kutoa tamko rasmi kuhusu matumizi ya mafuta
haya.”
Binafsi naona kuwa swali ambalo bado limebaki kwa
kipindi cha miaka inayokaribia 10 kwa sasa je kwanini Ocean Road kwa upande
wake na TFDA ya wakati huo kwa pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa nini kila
mmoja alipita njia yake katika hilo?
Kama hoja ni madhara mbona sigara, tumbaku, pombe
zina madhara kwa binadamu lakini hazijapigwa marufuku bali tu imekwa sentensi katika
bidhaa hizo kuwa zina athari kwa afya ya mtumiaji?
Kwa hakika hata kama kuna kemikali ndani ya mafuta
hayo, kwa maendeleo ya sayansi ya sasa inaweza kuondolewa kwa kutumia vifaa
bora ili kuisaidia jamii kuendelea kuyatumia mafuta hayo na hilo litasaidia
kukuza hata uchumi wa maeneo ambayo mibuyu inastawi kwa wingi.
Kwa maana ya mazungumzo ya ndugu hawa, wao walikuwa
wakitumia unga wa ubuyu na mafuta yake kama kiungo kwa miaka mingi wamezaliwa
wakiona mababu na mabibi wanautumia unga na mafuta hayo iweje ulipigwa
marufuku?
Mwanakwetu ushauri wangu hasa kwa Mkemia Mkuu wa
Serikali, Ocean Road na TFDA mpya ya sasa watoe wataalamu ambao ni wazaliwa wa
asili ya mikoa ya Dodoma, Singida na hata Iringa wakae pamoja walitazame jambo
hilo alafu watoke kuielezea jamii ya watumiaji wa kiungo hicho na hatua kadhaa
za maboresho ya kiungo hicho ili kuondoa utata kwani nimebaini kuwa kiungo
hicho bado kinatumika kwa siri.
Mwanakwetunalisema hilo kwa kuwa itambulike
waziwazi kunaga ubaga kuwa namna ya kupika na kula vyakula ni sehemu ya
utamaduni wa makabila yetu. Kupiga marufuku haitoshi, elimu ya kina inahitajika
zaidi isitoshe hata huko kupishana kwa wataalamu kunajenga hoja nyengine.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment