Adeladius Makwega-TANGA
Januari 10, 2024 Mwanakwetu alitumia muda wake mwingi
kutembelea maktaba ya familia yake ambayo ina mkusanyiko wa nyaraka nyingi ambazo kwa hakika zimehifadhiwa vizuri, ndani
yake zipo barua mbalimbali zilizowahi kuandikwa na wanafamilia, zipo picha,
kadi za kiliniki, vyeti vya kuzaliwa, mitihani , ripoti za shule, barua za
posa,vyeti vya ndoa, vyeti vya ubatizo, madaftari na shajara kadhaa tangu mwaka
1938.
Kwa hakika unapoingia katika nyaraka hizo mara nyingi
anayeingia huko hutekwa na mtu ambaye yu jirani naye kidamu, ambalo hilo halina
ubishi, hata Mwanakwetu lilimkumba.
Mwanakwetu alivutiwa na taarifa za watu wawili , mmoja yu hai
mwingine ni marehemu, jamaa hao wawili ni Mwalimu Francis Makwega na Mwalimu
Doroth Hezron Mlemeta, ambapo aliyehifadhi alimtambulisha kama Mwalimu Doroth
Makwega, hao ndugu wawili ni wazazi wa Mwanakwetu yaani baba na mama.
Mwanakwetu alitazama picha nyingi za mama yake na mwisho alivutiwa
na mwandiko wa mama mzazi yake alivyokuwa akiumba herufi.
Kwa kuwa huyu mama alishafariki, Mwanakwetu alihitaji
kuwalingishia watoto wake namna mama yake alivyokuwa akiandika.
Je mama huyu alikuwa na mwandiko mzuri kuliko wajukuu zake?
Kweli Mwanakwetu alikutana na shajara ya mwisho mwisho wakati
wa uhai wa huyu mama ambayo ilikuwa ya rangi bluu, ililiwa na panya kidogo,
lakini panya hao hawakuweza kuitafuna yote maana ilikuwa na gamba gumu.
Usalama wa shajara hiyo ulikuja baada ya kupatikana muda
mfupi baada ya mwalimu huyu kufariki dunia miaka 22 iliyopita na hapo ndipo
shajara hiyo ikabaki kuwa salama na kuhifadhiwa , hadi sasa Mwanakwetu
anaifungua na kuisoma.
Hapo Mwanakwetu akakutana na kipande cha shairi lililopewa
jina HUNA likiwa na bei tatu kama
unavyoliona na mama huyu kaandika kwa mkono wake mwenyewe, Mwanakwetu akasoma
alafu akacheka sana, hasahasa neno AMBI ikimanaanisha kitu cha urembo wapakacho
akina mama, kama piko kuongeza urembo, hivi sasa ni maarufu mno , bi harusi
hawezi kuolewa hadi apake AMBI.
Mwanakwetu akaendelea kuipekua shajara hii ya mama yake akakutana
na kurasa moja imeandikwa kwa wino mwekundu.
Hapo kunaonekana masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000
Ikieleza idadi ya vituo va kupiga kura-Jimbo la Ilala vilikuwa 265 na Jimbo la
Ukonga Vituo 719 jumla kuu kwa majimbo mawili ya wilaya ya Ilala ilikuwa na
vituo 982 , mwisho akaandika watu 4000, hiyo idadi 4000 haikufafanuliwa kama ilikuwa ni
idadi ya wasimamizi au nini?
Mwanakwetu akaendelea kupekua shajara hiyo akakutana na
karatasi nyingine ikiwa na maandishi ya Masharti ya Usimamizi wa Uchaguzi.
Katika kurasa hizo tatu tangu hii ya Masharti ya Usimamizi wa uchaguzi ,Idadi ya Vituo vya Kupiga Kura na
shairi la Huna , hayo mambo matatu yalimpa tafakari kubwa Mwanakwetu karibu
usiku mzima, akijiuliza ilikuwaje mama yake aliandika haya mambo katika shajara
yake ambayo leo hii miaka karibu 24?
Kwa hakika Mwanakwetu hakupata majibu
Mwanakwetu alikula chakula cha usiku huo na kulala vizuri,
kulipokucha tu alifungua simu yake ya kiganjani gafla alikutana na video katika
ukurasa wa Bibi Helen Kijo Bisimba ukiwa na akina wakilalamikia madhaifu ya
viongozi wetu.
“Hata mkisema tukapige
kura ,mnadhani tuna hamu tena ya kupiga kura? Wakisema tupige kura hatuna hamu
kweli. Naamka saa kumi na mbili nasema napigia kura watoto, wajukuu wangu waje
wanisaidie, sasa sioni hata hiyo faida ya kuamka asubuhi, sasa ninaamka kwenda
kufanya nini?”
Mwanakwetu alipowatazama akina mama
hao aliwalinganisha sawa sawa na mama yake mzazi kama angekuwa hai.Hapo hapo
Mwanakwetu akakumbuka yale mambo matatu katika shajara ya mama yake, ubeti wa
shairi,vituo vya kupiga kura na masharti ya usimamizi.
Mwanakwetu akasema,
“Mama yangu alikuwa anashiriki uchaguzi kama Msimamizi wa Uchaguzi
.”
Mwanakwetu akasema moyoni,
“Akina mama sasa wamekata tama, Rais wa sasa wa Tanzania ambaye
ni mwanamke anatakiwa afahamu kuwa Watanzania wamekata tamaa sana na hawana hata
hamu ya kupiga kura.Jukumu la Rais wa sasa wa Tanzania anatakiwa kutambua kuwa
anayo kazi ya kurejesha miiyo ya watu waliokata tamaa kama akina mama hawa.Rais
Samia anatakiwa kuweka viungo katika mioyo ya Watanzania ili wawe na hamu ya
kupiga kura . Kubwa CCM waache kuishi kimazoea kama walivyoishi zamani, maana
kama walizoea kupika chakula chuku chuku alafu kikaliwa basi sasa wakifanya
hivyo watapata tabu.”
Mwanakwetu akaendelea kusema moyoni,
“Kwa kuwa Rais wa sasa wa Tanzania ni mwanamke na ni mama anatakiwa
kila anachopika kisiende jamvini kuliwa bila ya kuwekewa viungo, kwa
kuwa rais wa sasa ni Mzanzibari, siri ya wanawake wa Zanzibari ni kupika kwa
kutumia viungo vingi hilo hapaswi kuachana nalo hata mara moja.”
Mwanakwetu akataja maana ya kupika
chakula chukuchuku,
“Ni kuishi kwa CCM kama ilivyokuwa ikiishi zamani, dhana mojawapo
ya kupika chukuchuku sasa CCM inasema fomu ya Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ndani ya CCM itakuwa moja. Huku ni kupika chakula
chukuchuku na kukiacha kiliwe. CCM iweke viungo vingine kwa ruhusu watu tofauti
waingie kilingeni, hilo pekee litaongeza ladha na hamu ya Watanzania kupiga
kura.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
“Rais Samia awaambie hao wanaotaka mgombea mmoja fomu moja,
kuwa yeye ni Mzanzibari chakula chake lazima kiwe na viungo ili kinoge.”
CCM ya samia isipofanya hivyo itakuwa inapika chakula chukuchuku na chakula hicho kitakuwa hakinong.
Hapo Rais Samia atakuwa hana cha kulingia na mwisho wake utakuwa mbaya kama lilivyo shairi kutoka shajara ya mama yake Mwanakwetu.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka Huna Mama Huna na Usikubali Chukuchuku.
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment